Marehemu amtaka chifu aliyemcharaza viboko amlelee mwanawe
MWANAFUNZI wa kidato cha kwanza aliyefariki kwa kunywa sumu Kisii amemtaka naibu chifu aliyemcharaza amlelee mtoto wake wa mwaka mmoja.
Marehemu Joyce Bonareri Otuke, 18, pia amemtaka afisa huyo wa serikali kuhudhuria mazishi yake na waombolezaji wengine kwa wingi atakapozikwa.
Haya ni kwa mujibu wa matakwa aliyoandika kwenye kijikaratasi alichokiacha kabla ya kunywa sumu iliyomsababishia mauti.
Mwendazake anasemekana kuchukizwa na kitendo cha naibu chifu wa kwao kijijini Amabuko, eneobunge la Nyaribari Masaba kumwahibu hadharani kwa kutoenda shule.
Alikuwa ameripotiwa kwa naibu chifu na wazazi wake.
Kulingana na Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Masaba Kusini Robert Kibuchi, wameanzisha uchunguzi wa kijikaratasi hicho ambapo anamshutumu afisa huyo wa serikali kwa “kusababisha” kifo chake.
“Msichana huyo aliacha notisi ambapo alimhusisha naibu chifu wa eneo lao kwa kumfanya anywe sumu, ambayo hatimaye ilisababisha kifo chake.
“Tunategemea sana kijibarua hicho kwa uchunguzi wetu. Ni tukio la kusikitisha ambalo limempata afisa wa serikali,” kamanda huyo aliambia Taifa Dijitali kwa njia ya simu.
Naibu chifu huyo alisimikwa siku chache zilizopita kuchukua wadhifa huo wa utawala.
Kijibarua hicho cha kurasa moja ambacho Taifa Dijitali ilifanikiwa kukiona, kiliandikwa kwa lugha za Ekegusii, Kiswahili na Kiingereza.
Kabla ya kunywa sumu hiyo, marehemu alipiga toba ya kufanya amani na Muumba wake na kudokeza kuwa anaelekea kwake Kristo.
“Nimeamua kumfuata Yesu. Kwa hayo yote umenitendea, uzidi kubarikiwa. Umeniadhibu mbele ya baba, mjomba na watu wengine,” inasema sehemu ya barua hiyo inayodaiwa kuachwa na mwanafunzi huyo aliyoiandikia naibu chifu
Marehemu aliweka wazi kwamba alikumbana na masaibu ya kutisha na kukejeliwa katika afisi ya msimamizi huyo alipokuwa akiadhibiwa.
Alidai aliitwa kila aina ya majina na kudhihakiwa kwamba alikuwa na hamu isiyoisha ya kuzuru nyumba za wavulana.
Aliongeza kuwa waliomuadhibu walichuma gugu moja linalowasha na kumwekea ili ahisi uchungu zaidi.
Kabla ya kunywa sumu, mama huyo wa mtoto mmoja alimuaga mwanawe na kumtakia aishi miaka mingi
“Mwanangu naomba ubaki na amani. Nitameza sumu ambayo nitainunua kwa sababu nilizozieleza. Nakuomba umtunze mtoto wangu vizuri na barua hii kufikie. Mimi sio wa kwanza kufa,” ilisema barua katika mwendelezo.
Kulingana na ripoti za kimatibabu katika hospitali ya Keroka ambapo mwathiriwa alikimbizwa, marehemu alimeza sumu ya kuua wadudu siku ya Alhamisi na kufariki dunia Jumamosi.
Mwili wake umehifadhiwa katika hospitali hiyo alikokimbizwa ukisubiri upasuaji.