MARY NJERI: Anafuata nyayo za Mama Kayai
Na JOHN KIMWERE
DAH! Wanasoka bora, waigizaji mahiri na wengineo duniani wametokea ghetto unaambiwa. “Bila shaka kumbuka mwigizaji wa kimataifa raia wa Ujerumani, Martin Lawrence, msanii wa hapa nchini, Simon Peter ‘Hopekid’ pia mwanasoka wa kimataifa Dennis Oliech walivyoanzia kukuza talanta zao,” anasema Mary Njeri Thuo.
Dada huyu ambaye ni miongoni mwa waigizaji wanaoibukia hapa nchini anasema mitaa ya mabanda ndiyo kiboko yao.
Anadokeza kuwa ghetto imebeba wavulana na wasichana wengi tu waliokirimiwa talanta mbalimbali. Anasema kunao wanaspoti, wasanii na wengineo lakini wamekosa ufadhili.
”Serikali inastahili kushirikiana na serikali za Kaunti kubuni miundo msingi mizuri kuelekea kuzinoa vipaji za chipukizi ili kuwasaidia kukwepa kujihusisha na makundi haramu kama GAZA ” anasema na kuongezea kuwa maisha magumu ya Ghetto ndiyo hupelekea wengi kujikuta kubaya bila kutarajia.
Mwaka uliopita, polisi waliuawa wasichana watatu waliokuwa warembo ajabu waliokuwa wanachama katika kundi hilo lenye makazi yake mtaani wa Kayole.
Hata hivyo, anavitaka vyombo vya habari kuzipatia kipaumbele filamu za nyumbani ili kuokoa maisha ya vijana wengi ambao hupoteza maisha yao kupitia bunduki. Aliambia ukumbi huu kuwa uhuru wa vyombo vya habari nchini ulitazamiwa kuunda ajira kwa vijana lakini sivyo.
“Ili kutoa ajira katika tasnia ya filamu wamiliki wa vituo vya runinga hapa nchini hawana budi kuanzisha vipindi zaidi kurusha kazi za wasanii wa nyumbani,” alisema.
Mwigizaji huyo anaziponda baadhi ya kampuni zinazotengeneza filamu za hapa nyumbani kwa kutolipa waigizaji baada ya kufanya kazi. Alifichua anakumbuka mwaka jana alifanya kazi na kampuni moja ila hadi leo hajawahi pokea malipo. Alikuwa kati ya waigizaji kwenye filamu ya Hisia ambayo hurushwa kupitia Ebru TV Kenya.
Kwa wasanii wa hapa nchini anasema angetaka kutinga hadhi ya Mama Kayai aliyekuwa akiigiza kwenye kipindi cha Vitimbi kilichokuwa kikirushwa kupitia kituo cha KBC. Akijibu swari kuhusu msanii wa kimataifa ambaye humpendeza kwa muvi alizoshiriki alipumua na kusema wacha tu.
”Ingawa nilikuwa nikishiriki michezo ya drama shuleni,bila kujisifia nilianza kupendezwa na kazi za Martin Lawrence akiwa mtoto.” Baadhi ya filamu zake, Martin Lawrence aliye mwigizaji na mtangazaji ni ‘Life,’ ‘Bad Boys Part1,’ ‘Blue Streak’, ‘ Black Knight’, ‘Big Mamas House,’ ‘Bad Boys,’ na ‘National Security,’ kati ya zingine.
Kando na sanaa, dada huyu huendesha biashara ya kuuza nguo za mitumba katika soko la Gikomba, Nairobi. Hayo tisa. Kumi ana historia yake kwa kuzingatia amepatia mengi ikiwamo kuajiriwa kama askari rungu(watchman) kuteswa siyo haba akifanya kazi kwenye hoteli moja nchini Dubai.
Akifunguka kuhusu aliyoyapitia alisema ”Maishani mwangu sitawahi kuabiri ndege kwenda Dubai tena, nilikwenda mara moja na kufunga safari zangu katika taifa hilo.”
Anashauri wenzake kwamba msichana anapokwenda katika taifa hilo ni bahati kurejea akiwa hai, kule hupitia mateso chungu mzima.
Mary Njeri 34, analenga kubalansi familia angalau akibarikiwa kumpata msichana kwani ameolewa na wamebarikiwa wavulana watatu. Anashauri vijana kufanya kazi kwa bidii na kujiwekea malengo katika shughuli zozote wanazotekeleza.