Mary Wambui ateuliwa serikalini
Na CHARLES WASONGA
ALIYEKUWA Mbunge wa Othaya Mary Wambui ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira (NEA).
Kwenye tangazo lililochapishwa katika gazeti rasmi la serikali toleo la Jumatatu, Oktoba 14, 2019, Waziri wa Leba Ukur Yatani alisema Bi Wambui atashikilia wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mwanasiasa huyo alichaguliwa mbunge wa Othaya mwaka 2013 na kuchukua pahala pa Rais mstaafu Mwai Kibaki ambaye alistaafu siasa baada ya kushikilia kiti hicho tangu 1974.
Hata hivyo, katika uchaguzi mkuu wa 2017 Bi Wambui alipoteza kiti hicho baada ya kubwagwa katika mchujo wa Jubilee na mwandani wa Bw Kibaki Gichuki Mugambi.
Baada ya kushindwa, Bi Wambui, aliamua kutotetea kiti chake kama mgombea wa kujitegemea.
Badala yake aliamua kujikita katika kampeni ya kumpigia debe Rais Uhuru Kenyatta ili achaguliwe kwa muhula wa pili.
Mamlaka ya NEA ilibuniwa baada ya Rais Kenyatta kutia saini mswada kuhusu ajira uliodhaminiwa na aliyekuwa Mbunge Maalum, na sasa Seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja.
Asasa hiyo ina wajibu wa kukusanya maaelezo au data zote kuhusu nafasi za kazi na watu wanaosaka ajira ili kuwasaidia wanaosaka ajira kupata kazi ama katika sekta ya umma au sekta binafsi.