Habari Mseto

Masaibu huku hospitali kuu ikifungwa bila notisi

September 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BONIFACE MWANIKI

WAKAZI wa Kyuso katika eneobunge la Mwingi Kaskazini, kaunti ya Kitui, wamelalamikia vikali hatua ya kufungwa kwa hospitali ya Kyuso Level 4 na serikali ya kaunti ya Kitui kutokana na kile kilichotajwa kuwa tishio la usalama kwa wafanyakazi wake.

Wakazi hao sasa wanataka kufunguliwa mara moja kwa hospitali hiyo ambayo wanasema ndio ya pekee katika eneobunge hilo.

Katika ilani kwa wafanyakazi wote hospitalini humo iliyoandikwa Jumanne, Septemba 3,2019, mkuu wa idara ya matibabu Daniel Musiani alisema hatua hiyo ya kufunga hospitali ghafla ilitokana na ghasia na ukosefu wa usalama hospitalini.

“Kufuatia vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana kwa waajiriwa wanaofanya kazi hospitalini, wizara ya afya katika kaunti imeamua kufunga taasisi hiyo kabisa tukisubiri uchunguzi wa vikosi vya usalama na kuhakikisha usalama wa waajiriwa wote wanaofanya kazi humu,” ilisema barua kutoka kwa Dkt Misiani Nicodemus.

Wakazi wa eneo hilo wamepuuzilia mbali madai kwamba, kuna ukosefu wa usalama eneo hilo na kusema kwamba wanaadhibiwa tu kwa kuitisha maendeleo kutoka kwa serikali ya Gavana wao Bi Charity Ngilu (pichani) ambayo kulingana nao, imelegea nyuma kimaendeleo.

Nicodemus Muthengi, mkazi wa Kyuso alisema hospitali hiyo ilifungwa kutokana na sababu duni na hivyo akawataka wakuu wa kaunti kufungua tena taasisi hiyo.

“Hatujui na hatujasikia kuhusu ukosefu wa usalama eneo la Kyuso. Tunataka hospitali hiyo ifunguliwe tena na kuanza kazi kwa sababu watu wengi wanateseka bila sababu yoyote,” alisema Muthengi

Vilevile, Nicodemus alisema hospitali zilizo karibu ni za kibinafsi na ni ghali mno kwa wakazi kuzimudu.

Rose Maluki, mfanyabiashara mjini humo alisema wanahofia kuwa Gavana Ngilu anawaadhibu tu wakazi wa eneo hilo kwa kuelezea wasiwasi wao kuhusu kiwango cha chini cha maendeleo ikilinganishwa na sehemu nyinginezo za kaunti ya Kitui.