Maseneta waitwa Ikulu kabla ya hoja ya kumfurusha Kindiki kujadiliwa
Na CHARLES WASONGA
MASENETA 55 wa mirengo ya Jubilee na upinzani Ijumaa wameitwa katika Ikulu ya Nairobi kuafikiana kabla ya hoja ya kumwondoa Naibu Spika Kithure Kindiki kujadiliwa na kuamuliwa.
Miongoni mwa maseneta waliohudhuria mkutano huo ni wale sita ambao walikwepa mkutano wa awali, ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta.
Wao ni Millicent Omanga, Falhada Iman, Naomi Waqo, Victor Prengei, Mary Seneta na Christine Zawadi ambao wameitwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya Jubilee ili waadhibiwe.
Hata hivyo, licha ya kuhudhuria mkutano huo wa Ikulu Seneta wa Meru Mithika Linturi amedinda kuunga mkono hoja hiyo akisema sharti “nipewe orodha ya makosa ya Kindiki niyachunguze kwanza kabla ya kufanya uamuzi.”
Mnamo Alhamisi, Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata aliwatumia ujumbe maseneta wote 38 wa Jubilee wakitakiwa kuhudhuria kikao maalum cha seneti na kuunga mkono hoja ya kumwondoa Kindiki.
Wale ambao watakosa kuhudhuria kikao hicho wanaweza kupewa adhabu ambayo inaweza kujumuisha kufurushwa kutoka Jubilee kulingana na kipengee 17 (2) na (3) kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.
“Msimamo wa chama ni kwamba kimepoteza imani na Naibu Spika na hivyo kinataka aondolewe. Kwa hivyo, sharti uhudhurie kikao maalum cha seneti na upige kura kulingana na msimamo wa chama,” Bw Kang’ata akasema katika barua yake.
“Tafadhali zingatia kuwa msimamo wa chama katika suala hili ni kuunga mkono hoja hiyo,” barua hiyo ikaongeza.
Kutokana na tishio hilo, wengi wa maseneta waliokuwa katika kambi ya Naibu Rais William Ruto wamebadili msimamo na kuamua kuunga mkono mrengo wa Rais.
Upande wa Dkt Ruto umeachwa na idadi ndogo ya maseneta ambao hawawezi kubatilisha uamuzi wa kumfurusha Kindiki.
Mrengo huo unahitaji idadi ya maseneta 23 kuangusha hoja hiyo ya Kang’ata.