Habari MsetoSiasa

Maseneta wakosa kuelewana kwa mara ya saba

August 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya saba Jumanne, maseneta walifeli kuelewana kuhusu suala ya mfumo wa fedha baina ya kaunti.

Hii ni baada ya maseneta 34 kupiga kura ya kuunga mkono hoja ya kuahirishwa kwa mjadala ili kutoa nafasi kwa mashauriano zaidi na maafikiano. Maseneta 26 walipinga.

Hoja hiyo iliwasilishwa na Seneta wa Elgeyo Marekwet Kipchumba Murkomen (Jubilee) aliyetaka wapewe muda zaidi wa kujadili suala kwa kina ili wakubaliane kuhusu mfumo ambao hautaleta mgawanyiko nchini.

“Ni aibu kwamba tumegawanyika kuhusu suala hili ilhali kila Mkenya anatizama Seneti kama bunge lenye viongozi walio na hekima, ambako mwenyekiti wa BBI Yusuf Haji anaketi; mwenzetu kama vile Wetang’ula (Moses) alikuwa wanachama wa Kamati ya Maridhiano 2008 na mmoja wetu ni mwanasheria mkuu wa zamani,” akasema.

“Hii ndio maana napendekeza tuahirishe suala hili ili tujadiliane zaidi. Tunafaa kuonekana tukiunganisha nchi sio kuligawanya kwa misingi ya wale wanaoongezewa fedha na wanaopokonywa,” akaongeza Bw Murkomen.

Kauli ya Bw Murkomen aliungwa mkono na maseneta Mohamed Faki (Mombasa), George Khaniri (Vihiga), Moses Wetang’ula (Bungoma) miongoni mwa wengine.

Bw Wetang’ula alisema ingawa kaunti yake ya itafaidi chini ya mfumo wa ugavi uliopendekezwa, kwa kuongezewa Sh930 milioni, hangependa kaunti zingine zipoteze fedha zozote.

“Sitaki tupitishe mfumo huu, kisha kaunti yangu ifaidi huku kaunti zingine kama Wajir na Mandera zipoteze takriban Sh2 bilioni kila moja kana kwamba hazina ndani ya Kenya,” akasema seneta huyo ambaye pia ndiye kiongozi wa Ford Kenya.

Lakini akipinga hoja hiyo Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata alisema alisema hiyo ilikuwa sawa na kuahirisha “shida” ilhali hawana uhakika iwapo litatanzuliwa.

“Tumechaguliwa kama viongozi kutatua shida za watu wetu. Kuahirishwa kwa suala hili kutafanya tuonekane kama viongozi wasioelewa majukumu yao,” akasema Bw Kang’ata.

Hoja hiyo ya Murkomen pia alipingwa na kiongozi wa wengi Samuel Pogishio na mwenzake wa wachache James Orengo.

Naibu Spika Profesa Margaret Kamar aliwataka viongozi wa pande zote kuandaa vikao vya maridhiano wiki hii ili maseneta wafanye kikao kingine Jumanne kukamilisha mjadala kuhusu suala hilo.