• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Mashahidi 68 kuitwa katika kesi inayomkabili Waititu

Mashahidi 68 kuitwa katika kesi inayomkabili Waititu

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) atawaita mashahidi 68 katika kesi ya ufisadi wa Sh580 milioni inayomkabili Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu.

Viongozi wa mashtaka Bw Nicholas Mutuku na Vincent Monda walimweleza hakimu mkazi Bw Thomas Nzioka wako tayari kuanza kuwasilisha ushahidi katika kesi dhidi ya Waititu, mkewe Susan Wangari Ndung’u na washukiwa wengine wanane waliokanusha kesi za utoaji zabuni ya ujenzi wa barabara kinyume cha sheria.

Kesi dhidi ya Bw Waititu aliyeshtakiwa Julai 29, 2019 itaanza kusikizwa kuanzia Januari 26 hadi Feburuari 6, 2020.

Mawakili Gitobu Imanyara, Mbiyu Kamau na wengine wanane walipendekeza kesi hiyo ianze Januari 2020 kuwawezesha wateja wao kuwarudisha watoto shule na kuenda sherehe za siku kuu ya Krismasi na Mwaka mpya wa 2020.

Viongozi wa mashtaka pamoja na mawakili hao walieleza mahakama wangelitaka korti izuru kaunti ya Kiambu kukagua miradi inayodaiwa ililipwa kiwango hicho kikubwa cha pesa.

“Afisi ya DPP itawasilisha mashahidi 68 ikiwa ni pamoja na wataalam watatu katika masuala ya fedha na masuala mengineyo ya utoaji huduma kwa umma,” alisema Bw Monda.

Kiongozi huyo wa mashtaka alieleza mahakama kuwa nakala za ushahidi zimekabidhiwa washtakiwa wote na iwapo watakuwa na swali afisi ya ODPP itajibu.

“Je, umepanga ratiba ya mashahidi namna gani,” Bw Nzioki alimhoji Bw Monda.

“Nitawaita mashahidi wakuu kwanza kulingana na orodha tuliyoandaa,” alijibu Bw Monda.

Mahakama ilifahamishwa mashahidi wakuu wote watafika kortini kwa viwango kulingana ushahidi watakaotoa.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa hao walithibitisha wamepokea ushahidi na wanaendelea kuukagua kwa lengo la kutambua iwapo uko sawa.

Tuhuma

Bw Waititu amekabiliwa na mashtaka ya ufisadi kwa kupokea pesa ‘alizojua’ zimetoka kwa hazina ya kaunti ya kugharimia ujenzi wa barabara.

Kandarasi iliyopelekea Bw Waititu kushtakiwa ni ya ukarabati wa barabara kwa gharama ya Sh588 milioni.

Kandarasi hiyo ilipewa kampuni ya Testimony Enterprises Ltd.

Ukarabati wa barabara hizo uligharimiwa na pesa za kipindi cha 2017/2018.

Ushahidi wa tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) ni kuwa kampuni ya Testimony Enterprise inamilikiwa na Bw Charles Chege na mkewe Bi Beth Wangeci Mburu ambao ni wandani wa gavana huyo.

Kampuni hiyo ililipwa kitita cha Sh Sh147.3 milioni.

Washtakiwa hao walikanusha mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana.

You can share this post!

Maafisa zaidi ya 20 wakamatwa, wengine kadha wasakwa na...

DAU LA MAISHA: Anafinyanga vijana kitabia na kabumbu

adminleo