• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Masharti makali kwa wakulima watakaolipwa na NCPB

Masharti makali kwa wakulima watakaolipwa na NCPB

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imeweka masharti makali kuhusiana na wakulima watakaolipwa mahindi waliyowasilisha kwa depo ya kitaifa ya NCPB.

Katika taarifa, waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa alisema wakulima wanafaa kujiwasilisha katika bohari ya NCPB walikowasilisha mahindi yao.

Lakini lazima wawe wamejaza fomu ya kudai malipo na wawasili katika depo hiyo wakiwa wamebeba kitambulisho cha kitaifa, cheti cha kuonyesha ni walipaji ushuru, picha ndogo ambazo zimeidhinishwa na chifu, tiketi ya daraja la kupima uzani, stakabadhi ya kuonyesha kuwasilishwa kwa mahindi yao na ithibati ya malipo ya mahindi (ikiwa yamelipwa).

Wakulima wanatarajiwa kufika katika depo kuanzia Jumatatu Agosti 20, 2018 kupokea malipo yao.

Ikiwa kampuni zilihusika katika utoaji wa mahindi kwa NCPB, zinafaa kuwasilisha cheti cha kuonyesha zimesajiliwa, cheti cha nambari ya kulipa ushuru, cheti cha kuonyesha ulipaji wa ushuru na Fomu CR 12.

Wizara ya Ugatuzi ilichukua usimamizi wa Hifadhi ya Kimkakati ya Chakula (SFR), hasa kutokana na malalamishi mengi, kwamba wakulima wengi waliowasilisha mahindi yao mwaka wa 2017/18 hawakuwa wamelipwa pesa zao ili wafanyibiashara walipwe.

Hili kukabiliana na changamoto hiyo, suala la mahindi linatatuliwa na wizara tatu, moja, ile ya Usimamizi wa Maeneo Kavu (ASAL), Wizara ya Kilimo, NSFRF na NCPB.

Wakulima na waliowasilisha mahindi wanadai serikali Sh3.5 bilioni na serikali imetoa Sh1.4 bilioni, kuambatana na bajeti ya 2018/2019, alisema Waziri wa Ugatuzi Bw Eugene Wamalwa.

You can share this post!

Wabunge wa Jubilee wanaohujumu kazi ya Rais wakejeliwa

Mkewe Waititu mashakani kwa kujenga bila leseni

adminleo