Mashirika yadai raia wanategwa kuunga BBI
Na VALENTINE OBARA
MASHIRIKA ya kutetea haki za binadamu yamedai waasisi wa Mpango wa Maridhiano (BBI) wamewekea raia mtego ili kupitisha marekebisho ya katiba.
Wakiongozwa na Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC), wanaharakati jana walisema mfumo wa ugavi wa fedha ambao umeibua utata umekusudiwa kutumiwa kushurutisha Wakenya kupitisha marekebisho ya katiba.
Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wangali wanasubiriwa kupokea ripoti ya BBI ambayo itatoa mwelekeo kuhusu marekebisho ya katiba yanayopendekezwa.
Mkurugenzi Mkuu wa KHRC, Bw George Kegoro, jana alisema katiba iliyopitishwa 2010 ilitoa mwongozo bora kuhusu ugavi wa fedha.
Kulingana naye, hakuna kizingiti chochote kisheria kuhusu ugavi wa fedha kwa hivyo suala hilo ambalo limekwama katika seneti halifai kutumiwa kuchochea marekebisho ya katiba.
“Hakuna dharura ya kubadilisha katiba kwa minajili ya kufanikisha ugavi wa rasilimali. Sisitizo kwamba katiba ikirekebishwa ndipo maeneo yatagawiwa fedha kwa njia ya haki ni mtego,” akasema.
Wiki iliyopita, Chama cha ODM kilikiri kwamba Bw Odinga alikuwa ameunga mkono mfumo wa kugawa fedha kwa kaunti uliowasilishwa katika seneti kwa sababu aliamini katiba itakapopitishwa, mfumo utabadilika na kutakuwa na mfumo mpya unaokubalika na wengi.
Akiongea katika afisi za shirika hilo jijini Nairobi, Bw Kegoro alidai kuwa mtazamo aina hiyo umekusudiwa kufanya BBI ipate uungwaji mkono kwa wingi.
Alisema kwa sasa hakuna haja kubadili katiba ambayo hata haijatekelezwa kikamilifu.“BBI ni mpango ambao madhumuni yake halisi yayako wazi. Unalenga zaidi kunufaisha watu wachache walio na ushawishi katika taifa hili.
Ili kuufanikisha, umma wanaambiwa tu eti watapata pesa zaidi. Hakuna uwazi kwamba kuna tatizo kwenye katiba ambalo linazuia fedha kufikia kaunti. Hii si sababu ya dharura kurekebisha katiba,” akasema.
Wakati huo huo, wanaharakati walimtaka Rais Kenyatta achukue hatua za haraka kuhusu madai ya ufujaji pesa za kukabiliana na janga la corona nchini.