Habari Mseto

Maskwota waililia serikali iwazime wanaomezea ardhi yao mate

April 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

MASKWOTA wapatao 10,000 kutoka vijiji 19 vya tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu Jumatano waliandamana kwenye barabara za mji wa Hindi kuishinikiza serikali ya kaunti hiyo kuvunja kimya chake kuhusiana na mahangaiko ambayo maskwota hao wamekuwa wakipitia mikononi mwa mabwanyenye wanaolenga makazi yao.

Maskwota hao kutoka vijiji vya Mkondoni, Shee Mgambo, Karafuu, Sina Mbio, Kwasasi, Bar’goni, Ungu, Kibokoni, Msumarini na sehemu zingine wanadai mabwanyenye wamekuwa wakiwatisha kuwafurusha kutoka kwa makazi yao kwa lazima, wakidai wao ndio wamiliki halisi wa ardhi husika.

Mabwenyenye hao wanadaiwa kujihami kwa hatimiliki feki, ambapo baadhi yao wamekuwa wakiweka seng’enge kuzingira baadhi ya nyumba za maswota hao, jambo ambalo maskwota wanasema linawakosesha amani.

Wakati wa maandamano hayo yaliyochukua zaidi ya saa tatu, maskwota walitapakaa kwenye barabara ya Hindi na kisha kufululiza hadi kwenye makao makuu ya Kaunti ya Lamu yaliyoko mjini Mokowe amnao in umbali wa zaidi ya kilomita 20 ili kuwasilisha vilio vyao kwa gavana.

Maskwota wanamtaka Gavana, Fahim Twaha kushirikiana na Tume ya Ardhi nchini (NLC) ili kuwagawanyia maskwota hao ardhi na kuwapa hatimiliki ili kulinda makazi yao.

Mmoja wa waandamanaji, ambaye pia ni mzee wa kijiji cha Mkondoni, Bw Hassan Chonde, alieleza kutoridhishwa kwao na jinsi serikali ya kaunti inavyonyamazia suala hilo licha ya kuwakosesha amani wanakijiji.

“Tumeamua kuandamana ili kuwasilisha kilio chetu kwa ulimwengu. Tumechoka kuhangaishwa kwenye makazi yetu na hawa mabwenyenye. Kila mmoja wetu hapa ameishi kwenye vijiji husika kwa zaidi ya miaka 10. Itakuwaje leo hii eti kwa sababu fulani yuko na hela, anavamia makazi yetu na kudai kuwa ni yake.

“Serikali kuu kupitia NLC ishirikiane na serikali yetu ya kaunti ili kutugawanyia ardhi zetu. Tunataka kuzilinda na kuziendeleza,” akasema Bw Chonde.

Bi Magdalene Kachimbi kutoka kijiji cha Shee Mgambo alieleza kushangazwa kwake na jinsi serikali ya kaunti ya Lamu imekuwa ikiendeleza usoroveya wa ardhi kwenye vijiji vingine mbali na Hindi.

Alisema kuna haja ya vijiji vya Hindi pia kuzingatiwa na kutekelezewa usoroveya ili kila mmoja apewe ardhi yake na hatimiliki.

“Sielewi kwa nini serikali ya kaunti imekuwa ikibagua eneo la Hindi katika usoroveya wa mara kwa mara unaotekelezwa hapa Lamu. Utasikia usoroveya unafanywa Pate, Mpeketoni, Kiunga, Mokowe, Kizingitini, Faza na sehemu zingine za Lamu lakini Hindi hakuna shughuli yoyote ya usoroveya imetekelezwa. Tunataka kumuuliza gavana wetu ana mpango gani kuhusu ardhi za Hindi,” akasema Bi Kachimbi.

Bw Shadrack Murimi aliiomba kaunti kushughulikia ardhi za Hindi ili kuepuka ghasia kutokea siku za usoni.

Alisema mabwenyenye wanaolenga ardhi zao wamekuwa wakiibuka na mbinu tofauti tofauti za kufurusha maskwota hao kwenye makazi yao kwa lazima, ikiwemo kuharibu mimea kwa kuiunguza moto.

“Wanyakuzi wa ardhi wamekuwa wakiweka moto mashambani na kuunguza mimea yetu na haya yote ni katika harakati za kutufurusha kwa lazima. Hatutakubali kuacha ardhi ambazo wengine wetu tumezaliwa tukiishi ndani. Kaunti iangazie hili kwani huenda vita vikazuka siku zijazo,” akasema Bw Murimi.

Vijiji vya tarafa ya Hindi vimekuwa vikilengwa na wanyakuzi kila mara kutokana na kwamba vijiji hivyo vinapakana na eneo kunakoendelezwa mradi wa ujenzi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) huko Kililana na Mashunduani.