Habari Mseto

Maswali mhudumu, mwanafunzi wakiteketea kwenye bweni la shule

Na MERCY KOSKEI September 25th, 2024 2 min read

MASWALI yamezuka kufuatia kisa ambapo mwanafunzi wa Kidato cha Nne na msarifu mwanagenzi waliuawa katika mkasa wa moto usiku katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Sacred Heart iliyopo Rongai, Kaunti ya Nakuru.

Wanafunzi wengine walikuwa wamehudhuria maombi moto huo ulipozuka Ijumaa usiku, Septemba 20, na kuteketeza bweni katika kisa ambacho kimeibua maswali kwa shule hiyo na familia za wahasiriwa.

Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Nakuru, Samuel Ndanyi, amesema uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha moto huo.

Utata umeibuka kuhusu walichokuwa wakifanya msarifu mwanagenzi, Peter Muhari, 24, na mwanafunzi Aron Kirui, 17, ndani ya bweni la wanafunzi, wakati wengine walikuwa wakishiriki sala za jioni kabla ya kwenda kulala.

Kachero aliyechelea kutajwa alisema usimamizi wa shule uliita maafisa wa zima moto walipogundua bweni linateketea.

Walipozima moto, waligundua miili miwili iliyoteketea kabisa.

Baada ya kuhesabu watu, wasimamizi wa shule waligundua miili ilikuwa ya mwanafunzi wa Kidato cha Nne na msarifu mwanagenzi.

Mwili wa mwanafunzi ulifanyiwa upasuaji Jumatatu huku jamaa wa familia yake walioshuhudia shughuli hiyo katika mochari ya Nakuru wakigubikwa na majonzi.

Baada ya upasuaji, mwili ulihamishwa katika Kaunti ya Kericho. Familia ilikataa kuzungumza na wanahabari.

“Baba ya mvulana anafanya kazi katika taasisi ya serikali. Anahofia iwapo familia itazungumza na wanahabari huenda wakaathiriwa na unyanyapaa au kuhatarisha kazi yake. Shule ilitufahamisha kuwa polisi wamechukua usukani wa suala hilo na wanafanya uchunguzi. Bado tunasubiri majibu kuhusu kilichotendeka,” alisema jamaa wa familia.

Shule ilifungwa kwa wiki moja Jumapili ambapo wanafunzi waliruhusiwa kwenda nyumbani kufuatia tukio hilo lililofanyika wiki chache baada ya mkasa sawa katika Shule ya Nyeri ya Endarasha ambapo wanafunzi 21 waliangamia.

Kulingana na Bw Ndanyi, wanafunzi kadhaa waliandikisha taarifa kabla ya kuachiliwa kwenda nyumbani ili kusaidia katika uchunguzi.

Mkuu wa polisi kaunti hiyo alisema mwalimu mkuu na walinzi waliokuwa kwenye zamu Ijumaa wameandikisha taarifa vilevile.

“Uchunguzi kuhusu kisa hicho unaoendelea. Tulizuru shule hiyo Jumamosi pamoja na vikosi vingine ili kutathmini hali. Baada ya mkutano tuliafikiana kuwaachilia wanafunzi waende nyumbani lakini ilibidi turekodi taarifa kutoka kwa baadhi yao,” alisema.

Alisema chanzo cha moto huo bado hakijagunduliwa.

Afisa huyo alisema kampuni ya Kenya Power imezuru shule hiyo kutathmini iwapo nyaya za stima zilikuwa na hitilafu mkasa huo ulipofanyika.