Habari Mseto

Matangazo ya uchezaji kamari ni marufuku – Serikali

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

BODI unayosimamia kamari imepiga marufuku utangazaji wa michezo ya kamari katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Katika tangazo la Jumanne Aprili 30, 2019, bodi hiyo, iliyo chini ya Wizara ya Masuala ya Ndani na Mipangilio ya Serikali, ilipiga marufuku utangazaji wa michezo hiyo kati ya saa kumi na mbili asubuhi hadi saa nne usiku katika vyombo vya habari.

Wamiliki wa kampuni za uchezaji kamari pia wanakatazwa kuweka mabango ya kutangaza michezo hiyo au kutumia watu wenye ushawishi mkubwa kwenye matangazo yao. Vile vile, walipigwa marufuku kutangaza kwenye mitandao ya kijamii.

“Imeamuliwa kuwa utangazaji wa aina yoyote ya uchezaji kamari lazima uidhinishwe na bodi na matangazo ya aina hiyo lazima yawe na onyo kuhusiana na athari za uchezaji kamari,” ilisema bodi hiyo katika tangazo lililotiwa sahihi .

Lilisema kuwa lazima watangazaji watahadharishe watumiaji wa michezo hiyo kuhusiana na utegemezi wa michezo hiyo.

“Onyo hilo linafaa kuwa thuluthi ya tangazo kamili na maandishi sawa,”alisema Liti Wambua, kaimu mkurugenzi wa bodi hiyo katika barua aliyoandikia vyombo vya habari ikiwemo Nation Media Group, Royal Media na Standard Media.

Wamiliki wa vyombo hivyo wana hadi Mei 30 mwaka huu kutekeleza masharti hayo kwa kusema uchezaji kamari unadhuru watumiaji.