Habari Mseto

Matatizo ya akili yazidi kutokana na sheria kali za coronavirus

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WATAALAMU wa afya ya akili wameitaka serikali kuweka mipango ya kupunguzia Wakenya msongo wa mawazo, inapopambana na virusi vya corona.

Hii ni kutokana na ongezeko la visa vya watu kujitoa uhai wakilalamikia hali ngumu ya maisha, kuongezeka kwa mizozo ya kinyumbani na wengi kulewa chakari nyumbani wakijaribu kujiondolea mawazo.

Mtaalamu wa saikolojia Prof Halimu Shauri, ameonya kwamba matukio aina hii yataendelea kushuhudiwa kama serikali haitajali kuhusu afya ya kiakili ya wananchi ikiwemo wanaowekwa karantini.

Alisema masharti makali kama yanayohitaji watu kutokongamana wala kukaribiana, kujifungua nyumbani, pamoja na hali ngumu za maisha ni sababu tosha za kufanya binadamu kutatizika kiakili, ingawa ni masharti muhimu kupambana na ueneaji wa virusi vya corona.

“Tumeathirika kihisia, kiuchumi na unapoambiwa ukae karantini, mara msikaribiane…unakosa ule usaidizi uliozoea kutoka kwa wengine. Hatuna marafiki wa kuzungumza nao tena,” akaeleza Prof Shauri.

Aliongeza kuwa watu wanapoachwa pweke huwa wanawaza sana kuhusu matatizo yanayowakumba kimaisha na kuchukua hatua zinazowadhuru.

Anusurika kifo

Mnamo Jumamosi mchana, mwanamume mwenye umri wa makamu alinusurika kifo katika Kaunti ya Nakuru baada ya kujirusha kutoka kwenye daraja la wapita njia katika barabara kuu ya Nakuru kuelekea Nairobi.

Marafiki wake walisema jamaa huyo alikuwa ni mhudumu wa hoteli mjini Nakuru na alishikwa na msongo wa mawazo aliposimamishwa kazi wakati biashara zilipoathirika na masharti ya kupambana na Covid-19.

Kisa hiki kilijiri siku chache baada ya kingine katika kijiji cha Wuoth Ogik, Kaunti ya Migori, ambapo mwanamke alimrusha mtoto wake mtoni kisha akajaribu kujitoa uhai.

Kulingana na walioshuhudia, mwanamke huyo alikuwa amelalamikia hali ngumu ya kiuchumi kutokana na janga la corona.

Katika Kaunti ya Nyandarua, mwanamume aliacha watu midomo wazi alipovaa gunia na kuandamana na binti yake mdogo hadi katika Hospitali ya JM Memorial akitaka mkewe atolewe hospitalini.

Alidai maadui wa kibiashara wa mkewe waliwadanganya polisi kuwa alisafiri Tanzania majuzi ndipo akawekwa karantini.

 

Ripoti za Samuel Baya, Waikwa Maina, Valentine Obara na Ian Byron