Habari Mseto

Matumaini Wakenya 300 kulipwa fidia ya Sh440b

August 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEVIN J. KELLEY akiwa NEW YORK, Amerika

MATUMAINI ya Wakenya 300 walioathiriwa na shambulio la kigaidi, llililotekelezwa katika balozi za Amerika nchini Kenya na Tanzania mnamo 1998, kupata fidia ya Sh440 bilioni yamefufuka baada ya Mahakama ya Juu nchini Amerika kukubali kushughulikia kesi yao.

Mahakama ya Juu ilisema kuwa, itaanza kusikiza kesi hiyo kuanzia Oktoba mwaka huu na kutoa uamuzi wake Juni mwaka ujao.

Mahakama inatarajiwa kuamua ikiwa serikali ya Sudan inafaa kuwalipa fidia Wakenya na Watanzania walioathiriwa na shambulio hilo la kigaidi.

Wakati wa makala ya 21 tangu kutekelezwa kwa mashambulio hayo jijini Nairobi, waathiriwa hao walitaka kulipwa fidia.

Mmoja wa waathiriwa hao, Bi Elizabeth Gitonga, aliitaka serikali ya Kenya kuwasaidia waathiriwa.

“Serikali ya Kenya inafaa kutupatia msaada hata kama ni kiasi kidogo cha fedha,” akasema katika hafla hiyo ambapo hakukuwa na mwakilishi yeyote wa serikali ya kitaifa au kaunti.

Kesi hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Juu ya Amerika baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali ombi la kutaka waathiriwa wa shambulio hilo walipwe fidia ya Sh440 bilioni mnamo 2017.

Mahakama ya mwanzo iliyosikiza kesi hiyo iliagiza kuwa Sudan ilipe fidia ya Sh590 bilioni kwa Wakenya na Watanzania walioathiriwa na na shambulio hilo la kigaidi.

Mahakama pia iliagiza Sudan ilipe Sh440 bilioni kama adhabu ya kusaidia magaidi kushambulia Kenya na Tanzania.

Lakini mahakama ya Rufaa iliidhinisha fidia ya Sh590 bilioni na kutupilia mbali adhabu ya Sh440 bilioni.

Tayari waathiriwa kutoka Kenya na Tanzania wamepewa sehemu ya Sh590 bilioni. Mawakili wa waathiriwa hawajafichua kiasi ambacho kila mwathiriwa alipokea.

Sasa wanataka Mahakama ya Juu iagize Sudan kulipa fidia ya Sh440 bilioni kwa kufadhili magaidi waliolipua balozi za Amerika jijini Nairobi na Dar es Salaam miaka 21 iliyopita.

Watu 570 wameorodheshwa kama walalamishi katika kesi hiyo itakayosikilizwa katika Mahakama ya Juu.

Walalamishi zaidi ya 300 ni Wakenya, 80 ni raia wa Tanzania na waliosalia ni raia wa Amerika.

Wote hao walikuwa wafanyakazi katika balozi za Amerika jijini Nairobi na Dar es Salaam. Wengine walikuwa wanakandarasi waliokuwa wakihudumu katika balozi hizo.

Wengi wa watu 224 waliouawa katika shambulio hilo lililotekelezwa kwa mpigo katika balozi mbili za Amerika nchini Kenya na Tanzania mnamo Agosti 7, 1998, hawakuwa wafanyakazi au wanakandarasi katika balozi hizo.

Waathiriwa 214 waliofariki walikuwa wapita njia au walikuwa wakifanya kazi katika majumba yaliyokuwa karibu.

Mawakili wa washukiwa walishtaki Sudan katika mahakama ya Amerika kwa sababu nchi hiyo ilihusika katika kumpatia hifadhi kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaida Osma Bin Laden. Inadasadikiwa kuwa mashambulio hayo yalipangiwa nchini Sudan.

“Sudan ni sharti ilipe adhabu hiyo kwa kusaidia magaidi kutekeleza mashambulio,” akasema Gavriel Mairone, wakili kutoka jimboni Chicago, Amerika anayewakilisha waathiriwa.

“Sudan inafaa kuwalipa waathiriwa ndipo iondolewe na Amerika katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi duniani,” akasema Mairone.

Kundi jingine la waathiriwa 2,400 pia limewasilisha kesi kortini dhidi ya serikali ya Iran inayodaiwa kufadhili kundi la Al-Qaida.

Maelezo zaidi na AGEWA MAGUT