• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Mau Mau walia watambuliwe kisheria kwa ‘kumwaga damu’ kuikomboa Kenya

Mau Mau walia watambuliwe kisheria kwa ‘kumwaga damu’ kuikomboa Kenya

Na PETER MBURU

WAZEE wa Muungano wa Mau Mau, ambao ulipigania ukombozi wa Kenya kutoka mikononi mwa wakoloni sasa wanataka taifa kutambua muungano wao kisheria, kama ambao ulipigania uhuru wa taifa.

Wazee hao wameandikia bunge mswada, wakipendekeza kuwa kutokana na damu waliyomwaga, watu kufa na kuteswa, jambo la busara kwa serikali kufanya ni kuwatambua kisheria, ili waridhike.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa muungano wao Gitu Wa Kahengeri, wazee hao Jumanne walikutana na kamati ya bunge kuhusu Michezo, Utamaduni na Utalii ambapo waliieleza kuhusu sababu za kutaka watambuliwe.

Wazee hao walisema kuwa japo katiba ina vipengee fulani ambavyo vimetambua mashujaa kwa kazi yao ya kulifaa taifa, hakuna popote ambapo waliopigania uhuru wa Kenya wametajwa moja kwa moja.

“Tunachotaka ni kutambulika kupitia Sheria ya Bunge kuwa muungano wa MauMau ndio ulimwaga damu ukipigana kuikomboa Kenya kutoka mikono ya wakoloni,” Bw Wa Kahengeri akasema.

Wazee hao aidha walikumbwa na kibarua kigumu kutoka kwa wabunge kuhusu jina ambalo wanapendekeza litumiwe katika utambulizi huo la ‘Mau Mau War Veterans Association’, viongozi hao wakihoji kuwa muungano wa Mau Mau ulikuwa tu mmoja wa mingi iliyofanya kazi hiyo nchini, na kuwa unaleta dhana ya muungano wa eneo la Mlima Kenya.

Mzee Gitu Wa Kahengeri alipoongoza wanachama wengine wa Muungano wa Mau Mau kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Michezo na Utamaduni Machi 12, 2019. Picha/ Peter Mburu.

Vilevile, wizara ya Michezo na Utamaduni haijachangamkia wazo la wazee hao, lakini ikieleza kuwa vipengee fulani vya katiba vinaweza kurekebishwa na kuongeza sehemu inayotaja jina la kundi la waliohusika kupigania uhuru wa taifa, badala ya kuingiza kipengee kipya.

Katibu katika wizara hiyo Josephta Mukobe alifika katika kamati hiyo ya bunge sheria kuhusu mashujaa wan chi inaweza kufanyiwa marekebisho ambapo maombi ya muungano huo yatajumuishwa, lakini tu pale hawajatajwa.

“Tayari katiba imewatambua wapiganiaji uhuru, labda paongezwe kipengee kinachotaja muungano wao, lakini kwa jina la kuunganisha taifa,” akasema Bi Mukobe.

Wazee hao wanasema ni vibaya kuwa serikali ya Uingereza tayari imetambua Muungano wa Mau Mau kama uliopigania uhuru wa Kenya, lakini serikali ya Kenya takriban miaka 60 baadaye haijafanya hivyo.

“Katiba inasema tu wale walipigania uhuru, haisemi ni kina nani. Ni nani hawa?” Bw Wa Kahengeri akaeleza kamati hiyo ya bunge.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka alisema wanachama wa kamati hiyo watajadili na kutafiti suala hilo kasha kuja na mapendekezo ya mwisho.

Katika sehemu ya mwanzo ya katiba, wapiganiaji uhuru wa Kenya wametambuliwa wakiwa wa pili, baada ya Mungu. Hata hivyo, wazee hao wanadai kuwa hilo halitoshi, wakitaka jina la muungano litambuliwe kisheria.

You can share this post!

Kagame na Museveni wazidi kupakana tope

Washukiwa wa ubakaji waachiliwa, korti yasema sura ya...

adminleo