Habari Mseto

Mbegu bandia zimefurika madukani, Kephis yaonya

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAIKWA MAINA

WAFANYABIASHARA walaghai wameanza kusambaza mbegu bandia katika eneo la Bonde la Ufa huku msimu wa upanzi ukikaribia.

Aidha, meneja wa Idara ya Huduma za Mimea (Kephis) katika ukanda wa Bonde la Ufa Kiruri Mwangi ameonya kuwa matapeli hao wanatumia mifuko ya kampuni zilizoidhinishwa kuuza mbolea bandia.

“Kuna kiasi kikubwa cha mbegu bandia zinazouziwa wakulima. Tayari tumekamata washukiwa kadhaa na kuwafikisha mahakamani,”akasema Bw Mwangi.

Meneja wa Kephis aliyekuwa akizungumza katika eneo la Ol Joro Orok, alikiri kuwa ni vigumu kutofautisha kati ya mbegu bandia na zilizoidhinishwa.

Alitoa mfano wa washukiwa wa utapeli waliokamatwa waliokuwa wamepakia mbegu za sukumawiki ndani ya mfuko uliokuwa umeandikwa ‘mbegu za nyanya’.

“Baada ya kuzifanyia majaribio katika maabara, tulibaini kuwa rangi ya mbegu hizo ilikuwa tofauti na hazikuwa zikiota,” akasema Bw Mwangi.

“Tunawashauri wakulima kununua mbegu zilizoidhinishwa. Kabla ya kununua wanafaa kuangalia ikiwa mfuko wa mbegu una nambari maalumu ya utambulisho,” akaongeza.

Wakulima wanatakiwa kutuma nambari hiyo kwa Kephis ili kuthibitisha ikiwa mbegu wanazotaka kununua ni halali au la.

Aliyataka maduka ya pembejeo za kilimo kununua mbegu kutoka kwa wasambazaji walioidhinishwa na kuhakikisha kuwa wanapewa risiti baada ya kununua.

Bw Mwangi alisema kuwa wengi wa washukiwa waliokamatwa walidai kuwa hawakujua kwamba mbegu wanazouza ni bandia.

“Hiyo inamaanisha kwamba wenye maduka wanauza mbegu bila kuthibitisha ikiwa ni bandia au la na hivyo kujipata pabaya. Kwa bahati mbaya huwa tunawakamata ikiwa wameuza kiasi kikubwa cha mbolea,” akasema.

Bw Mwangi alisema idara ya Kephis imeimarisha vita dhidi ya watapeli wanaouza mbegu ghushi ambazo huenda zikachangia kupungua kwa mavuno na kusababisha baa la njaa nchini mwaka huu.

“Tuna maabara za kutosha zilizo na vifaa vya kisasa vya kupima ubora wa mbegu. Miongoni mwa maabara hizo ni ile ya Sh250 milioni iliyozinduliwa mwaka jana kwa lengo la kuhakikisha kuwa mbegu zinafikia viwango vya ubora vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa na Bara Ulaya,” akasema Meneja huyo.