Mbosso avunja nyoyo za mashabiki sababu ya malipo
Na CHARLES LWANGA
MAMIA ya watu waliohudhuria tamasha za kitamaduni za Malindi waliachwa wakisononeka baada ya msanii wa bongo ‘Mbosso’ kukosa kutumbuiza kwa madai ya kutolipwa na waandalizi wa tamasha hiyo.
Watu hao walipiga kelele na kurusha chupa za maji na pombe kwenye jukwaa baada ya msanii kutoka nchini Tanzania Mbwana Yusuph Kilungi almaarufu ‘Mbosso’ kukosa kuwatumbuiza katika hoteli ya Ocean Beach Resort mjini Malindi.
Shida ilianza baada ya waandalizi wa tamasha hiyo ambao ni wanabiashara mjini Malindi pamoja na wahisani wa tamasha kutoka Nairobi kukosa kumlipa msanii huyo kabla ya kutumbuiza kama walivyokubaliana.
Baadhi ya waandalizi ni Bi Maureen Awuor ambaye ni meneja wa Ocean Beach, Bw Nick Angore (mkurugenzi wa Budhas Lounge), Bw Zakayo Kaibunga (Mkurugenzi wa Budhas Lounge), Bw Samuel Kisandu (Mshawishi) na Bw Rodgers Kaibunga na wengineo.
Baadhi ya waandalizi waliambia Taifa Leo kuwa walikuwa wanafaa kumlipa msanii huyo Sh1.5 milioni lakini walilipa Sh1.2 milioni pekee, hatua ambayo ilimlazimisha mwanamuziki huyo wa Wasafi Classic Baby (WCB) kukataa kupanda jukwaani.
“Waandalizi pia walitoza ada za Sh1,000 hadi Sh5,000 ambayo ilikuwa ghali sana wakiwa na matumaini ya kuunda faida msimu huu wa Pasaka baada ya Churchill kuvuna pesa nyingi katika mji huo majuzi,” alisema.
Baadhi ya mashabiki walisafiri kutoka kaunti za Mombasa, Kwale, Taita Taveta na Tana River kujivinjari na kumtazama msanii huyo wa wimbo ‘hodari wa mapenzi.’
Baadhi ya wageni waheshimiwa akiwemo Gavana Amason Kingi na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho waliodaiwa kuwasili katika hoteli hiyo kuhudhuria tamasha hiyo walisusia kuketi kwenye viti vyao.
Msanii Susumila ambaye alikuwa anafaa kutumbuiza wakazi kabla ya Mbosso pia alisusia kutumbuiza baada ya waandalizi kukataa kuwalipa.