• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Mbunge adai maisha yake yamo hatarini

Mbunge adai maisha yake yamo hatarini

Na GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Mbunge wa Samburu Kaskazini Alois Lentoimaga sasa anadai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Akizungumza nyumbani kwake mjini Maralal, Bw Lentoimaga amedai kuwa kuna makundi ya uhalifu ambayo yanafadhiliwa na wanasiasa ili kuangamiza watu wasiokuwa na hatia eneo la Baragoi.

Alisema kuwa yeye na familia yake hawawezi kusafiri kuelekea Baragoi kwa sababu hana uhakika wa usalama wake kwani mashambulizi na mauaji ya kikabila yamekithiri.

Alishutumu maafisa wa polisi kwa kushindwa kuyakabili magenge ya uhalifu yanayohangaisha watu eneo la Baragoi.

“Imefikia wakati siwezi kuenda Baragoi kama mbunge wa maeneo hayo kwa sababu ni hatari. Naogopa naweza kuawa. Na nikiuawa sidhani kama familia yangu itapata haki kwa sababu wale wote ambao wameuawa hapa, familia zao hazijapata haki,” alisema Bw Lentoimaga.

Alishangaa ni vipi maafisa wa usalama wameshindwa kuwakamata hata mwalifu mmoja kwa kipindi chote mauaji yanaporipotiwa eneo hilo.

“Wanatuambia mkono ya serikali ni mrefu lakini inakuwa fupi ikifika Baragoi ama pengine hiyo mkono hakuna,” aliongeza.

Mbunge huyo mwenye utata alisema kuwa utovu wa usalama ambao umekithiri unachangiwa na serikali kushindwa kurudisha mifugo ambao huibwa kila mara.

“Wakati watu wengine wanang’a ng’ana kuzima ugonjwa wa Corona, watu wa Samburu wanauana wenyewe na serikali imenyamaza tu. Kwani Baragoi si Kenya? Serikali itamaliza lini maafa Baragoi?” Alishangaa Bw Lentoimaga.

Kulingana na Mbunge huyo, wakazi wa Samburu wanaishi kwa hofu ya mauaji ya mtutu wa bunduki kuliko tishio la ugonjwa wa Corona. Alisema kuwa zaidi ya watu 30 wameuliwa kinyama chini ya miezi mitano pekee.

“Kazi ya maafisa wa polisi imebaki tu kuokota miili ya wafu na kuchukua mochari,” aliongeza.

Watu wawili wameuawa kwenye visa viwili tofauti chini ya majuma mawili eneo la Baragoi, na maafisa wa polisi wanahoji kwamba visa hivyo vimetokana na uhasama wa kikabila.

You can share this post!

KAFYU: Dereva aua polisi akihepa kunaswa na polisi mwingine

Ruto azidi kutumia Twitter kupinga mabadiliko katika chama...

adminleo