• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mbunge adai Moi alitawazwa na matapeli

Mbunge adai Moi alitawazwa na matapeli

Na DENNIS LUBANGA

MBUNGE wa Mlima Elgon Fred Kapondi, amepuuzilia mbali hatua ya baadhi ya wazee wa jamii ya Wasabaot kumtawaza Seneta wa Baringo Gideon Moi kuwa kiongozi wa jamii ya Wakalenjin.

Mwenyekiti huyo wa chama cha Kanu, alitawazwa na wazee hao kuwa mwaniaji wa urais 2022, Jumamosi iliyopita. Wazee hao pia walisema kuwa Bw Moi ndiye ana uwezo wa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapokamilisha muhula wake wa pili 2022.

Hafla ya kumtawaza Bw Moi ilifanyika katika eneo la Kapsokwony baada ya seneta huyo kuhudhuria ibada katika Kanisa la Kapsokwony Seventh-day Adventist.

Wazee hao walimvisha kofia ya kitamaduni iliyoonyesha kwamba amepewa mamlaka na mkuki ambao ni ishara ya uongozi miongoni mwa jamii za Wakalenjin. Kutawazwa huko pia kunaashiria kuwa kiongozi yuko tayari kuongoza na kulinda jamii.

Ni mtu mmoja tu ambaye hutawazwa kuongoza jamii kwa muda fulani.

Aliyekuwa mbunge wa Mlima Elgon, Bw John Serut, kiongozi wa Chama cha Mashinani, Bw Isaac Ruto pamoja na viongozi kadhaa wa eneo hilo walihudhuria hafla hiyo.

Lakini Bw Kapondi ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais William Ruto alitaja kutawazwa kwa Bw Moi kama ‘kupoteza wakati’ akishikilia kwamba Naibu wa Rais hatalegeza kamba katika harakati zake za kutaka kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Kapondi alisema Dkt Ruto anaendelea na shughuli ya kuanzisha miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini na hatashiriki siasa za ushindani na Bw Moi.

Bw Kapondi pia alidai kuwa wazee waliomtawaza Bw Moi kuwa kiongozi wa jamii ya Wakalenjin si Wasabaot bali walikuwa matapeli wa kisiasa kutoka nje ya eneo hilo.

“Mimi nikiwa mwakilishi wa watu wa Mlima Elgon nasisitiza kuwa eneo hili linaunga mkono Dkt Ruto na Bw Moi asipoteze wakati na fedha zake kuendesha kampeni hapa,” akasema Bw Kapondi.

“Yeye (Bw Moi) ni seneta tu ambaye anafaa kushughulikia masilahi ya watu wa Baringo badala ya kuhadaiwa na walaghai wanaomezea mate fedha zake,” akaongezea.

Bw Kapondi alisema kuwa Bw Moi hatapata kura katika eneo la Mlima Elgon hata baada ya kutawazwa wikendi iliyopita.

“Ni jambo la kushangaza kwamba wazee ambao wanajali masilahi ya matumbo yao wanamhadaa Bw Moi kuwa wanaweza kumfanya kuwa kiongozi wa jamii wa Wakalenjin,” akaongeza.

“Baadhi yetu bado wanashangaa jinsi wazee wachache wenye njaa na haja ya kujaza matumbo yao wanaweza kumdanganya Bw Moi kuwa atakuwa Rais. Hilo linawezekana kweli?” akauliza.

Mbunge huyo pia alisema Dkt Ruto tayari alitawazwa kama mzee wa Sabaot katika eneo la Cheptais, Mlima Elgon mwaka jana kwenye sherehe iliyojaa shamrashamra nyingi iliyohudhuria na umati mkubwa.

You can share this post!

Wamiliki vyombo vya habari waonywa dhidi ya kudunisha...

Wezi waiba kahawa ya Sh400,000 kiwandani

adminleo