Mbunge ahimiza vijana watumie ubunifu kujiendeleza
Na LAWRENCE ONGARO
MBUNGE wa Thika Bw Patrick Wainaina alipendezwa na akaelezea kufurahishwa kwake na ubunifu uliofanywa na vijana watano waliounda kibanda maalum cha kunyunyuzia dawa ya kuzuia viini wakati huu dunia inakabiliana na janga la Covid-19.
Kibanda hicho ni cha kipekee ambacho watu wanapita ndani huku kikipuliza dawa hiyo kama mojawapo ya tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Vijana hao kutoka kanisa la PCEA Makongeni, Thika wameonyesha wazi kuwa ubunifu pia ni talanta ya kipekee.
Bw Wainaina alisema vijana hao wanastahili kupewa motisha zaidi ili waweze kujiendeleza katika hatua nyingine.
Ili kuonyesha ukarimu wake kwa vijana hao, mbunge huyo aliwapa Sh50,000 zitakazowasaidia kujiendeleza zaidi.
“Nimeridhishwa na ujuzi wa hali ya juu wa vijana hawa chipukizi,” alisema Bw Wainaina.
Kiongozi wa vijana waliounda kibanda hicho, Eric Karau Ng’ang’a alisema lengo lao kuu lilikuwa ni kwa minajili ya kupambana na Covid-19.
“Mimi nimesomea uhandisi wa umeme katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, na kwa hivyo niliona ni muhimu tushirikiane na vijana wenzangu ili kuunda kibanda hicho,” alisema Bw Ng’ang’a.
Alisema kuunda kibanda hicho kimewagharimu Sh138,000 na wakipewa ufadhili zaidi wanaweza kuunda vingine.
“Tutaendelea kuunda vingine tukipata ufadhili zaidi na kibanda hiki kinastahili kuwekwa pahala ambapo kuna watu wengi kama sokoni, makanisani, vituo vya magari na sehemu nyinginezo za umma,” alifafanua Bw Ng’ang’a.