Habari Mseto

Mbunge afukuzwa bungeni kwa kuingia na mtoto

August 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kwale katika Bunge la Kitaifa, Zulekha Hassan amesababisha kioja Jumatano asubuhi alipoingia kwenye ukumbi wa mjadala bungeni huku akiwa amembeba mtoto mdogo mikononi mwake.

Shughuli za bunge zilisimama kwa muda wa robo saa huku wabunge wakitoa hisia mseto kuhusiana na kitendo hicho.

Kiongozi wa wengi Aden Duale ambaye alikuwa akichangia mjadala kuhusu mzozo kati ya Kenya na Somalia kuhusu eneo la mpaka baharini alilazimika kukatiza mchango wake.

“Mheshimiwa Spika, Bi Zulekha amevunja sheria za bunge kwa kuingia ukumbi akiwa amembeba mtoto. Kwa nini aliruhusiwa kuingia ukumbuni na mtoto,” akasema Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini.

Hapo ndipo Spika wa muda Chris Omulele aliwaamuru walinzi wamwondoe nje mbunge huyo.

“Naamuru walinzi wamwondoe Bi Zulekha Hassan nje kwa kuvunja sheria za bunge. Hata kama ana haki ya kumtumza mwanawe, hafai kufanya hivyo ndani ya ukumbi wa bunge,” amesema Omulele.

Baada ya amri hiyo wabunge walizua vurugu ukumbini huku wabunge wanawake wakipinga kufurushwa kwa Bi Hassan na wenzao wakiume wakiunga mkono amri hiyo.

Mbunge wa Alego Usonga, Sam Atandi ni miongoni mwa wabunge wachache wa kiume waliomtetea Bi Hassan.

Mbunge huyo pia alifurushwa alipojaribu kuwazuia walinzi waliokimsindikiza nje mbunge huyo mwakilishi wa Kwale.

Akiongea na wanahabari baada ya kuondoka ukumbini, Bi Hassan amesema alimleta mwanawe bungeni “kwa sababu ya dharura iliyonipata asubuhi”.

“Nilikuwa na dharura fulani ndipo nikaamua kuja na mtoto wangu kazini. Sifai kufurushwa kwa sasa mtoto wangu sio bomu la kiatomiki na hawezi kulipuka.” akasema.

Mbunge wa Ijara, Sophia Abdi Noor naya amesema inasikitisha kuwa tukio kama hilo linaweza kushuhudiwa bungeni ambako sheria zinatungwa.

“Mtoto huyu ana haki. Ikiwa bunge halitatenga chumba maalumu ambapo wanawake wote wenye watoto wachanga watawanyonyesha, basi tunawahimiwa wenzetu wenye watoto wadogo kuja nao bunge. Hii ndio njia ya kipekee ya kupitisha ujumbe kwamba tunafaa kutungewa chumba cha kuwanyonyesha watoto wetu,” akasema.

Naye mbunge wa Laikipia Kaskazini Sarah Korere (ambaye amebeba pichani) alisema kila mtoto ana haki ya kunyonya kwa miezi sita ya kwanza.

“Wabunge wa kike sharti wawe mstari wa mbele kutii kanuni hii muhimu katika afya ya watoto,” akasema.

Mnamo 2013 wabunge walipitisha hoja iliyopendekeza kwamba Tume ya Huduma za Bunge (PSC) itenge chumba maalum katika majengo ya bunge ambamo wabunge wa kike watakuwa wakiwawanyonyesha watoto wao.

Lakini tangu hilo hajatekelezwa hadi sasa.