Habari Mseto

Mbunge alia kuna njama ya kumnyima Kindiki unaibu rais

Na DAVID MUCHUI October 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Imenti ya Kati Moses Kirima sasa anadai kuwa kuna njama inayosukwa ya kuhakikisha kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki hapokezwi unaibu rais iwapo Rigathi Gachagua ataondolewa afisini.

Bw Kirima amedai kuwa wabunge wa Mlima Kenya waliunga mkono hoja ya kumtimua Bw Gachagua kwa ahadi kuwa Profesa Kindiki angepokezwa wadhifa huo lakini sasa mambo yameanza kubadilika.

Wiki hii Bw Gachagua atafahamu hatima yake wakati ambapo maseneta wanatarajiwa kupiga kura ya kuunga au kupinga hoja dhidi yake baada ya Bunge la Kitaifa kumwondoa madarakani.

Suala la mrithi wa Bw Gachagua limeshuhudia mgawanyiko mkubwa hasa baada ya baadhi ya wanasiasa Magharibi kutaka nafasi hiyo itunukiwe Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi au Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.

Kwenye ukanda wa Mlima Kenya,  magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Irungu Kangáta (Murangá) na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ni kati ya wale wanaongángánia wadhifa huo na wanatoka eneo la Mlima Kenya Magharibi.

Bw Kirima Jumatatu alisema wengi kumezea mate wadhifa huo ni jaribio la kughairi ahadi ambayo ilitolewa kwa wanasiasa kutoka Ukanda wa Mlima Kenya hasa eneo la Mashariki anakotoka Profesa Kindiki.

“Mimi nilikuwa mtu wa mwisho kuunga hoja ya kumtimua Bw Gachagua kwa sababu niliulizwa kwa nini sitaki Kindiki ambaye ni jirani yangu awe naibu rais,” akasema.
Mbunge huyo alisema amekabiliwa na raia waliotaka kujua kwa nini aliunga mkono hoja ya kumwondoa mamlakani Bw Gachagua. Alisema alihakikishiwa kuwa  Profesa Kindiki angepokezwa wadhifa huo.

“Tunahisi kuwa tulihadaiwa kwa sababu sasa watu wengi wanaendelea kujitokeza. Tulipoambiwa tutie saini hoja hiyo ni jina la Profesa Kindiki pekee lilitajwa  kama atakayechukua wadhifa wa naibu rais,

“Hii ndiyo maana tulimwondoa Gachagua lakini sasa kila eneo linataka wadhifa huo,” akaongeza.

Aliwahakikishia raia kuwa iwapo sasa Profesa Kindiki hatakuwa naibu rais, basi watashirikiana na maseneta kuangusha hoja ya kumtimua Bw Gachagua.

“Kama wabunge wa Meru tulikuwa tumefurahi kumtimua Gachagua ili Kindiki awe naibu rais. Kama tumechezwa, tutashinikiza maseneta waangushe hoja hiyo na tutangaze kwenye vyombo vya habari kuwa tulihadaiwa,” akasema.

Vilevile mbunge huyo alimwepushia Rais William Ruto lawama kuhusiana na masaibu ya Bw Gachagua akisema kuwa ahadi kuwa  Profesa Kindiki angekuwa naibu rais, ilitosha kuwashawishi waunge hoja dhidi ya naibu rais.

“Hatuna amani na tunamwomba Rais Ruto awapuuze wale wanaotaka kuwa naibu rais na atoe wadhifa huo kwa Profesa Kindiki jinsi tulivyoahidiwa. Ukweli ni kuwa kuna wabunge wengi sasa wanapigia upato watu kutoka jamii zao,” akasema.

Wabunge wote 11 kutoka Kaunti ya Meru pamoja na wenzao wanne kutoka Tharaka-Nithi waliunga mkono hoja ya kumtimua Bw Gachagua.  Kwenye gatuzi la Embu, ni wabunge watatu pekee walipinga hoja ya kumtimua Bw Gachagua.