Mbunge apendekeza pesa zaidi kwa kilimo
ONYANGO K’ONYANGO na BARNABAS BII
MWENYEKITI wa kamati ya Kilimo katika Bunge la Kitaifa, Bw Sila Tiren, ameirai serikali kuu iongeze kiasi cha fedha kwenye bajeti kinachotengewa sekta hiyo hadi asilimia 10.
Hatua hiyo alisema itasaidia kuongezea nchi mapato. Bw Tiren alisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na kuongezea taifa uzalishaji wa vyakula vya kutosha.
Pia mgao mkubwa wa kifedha kwa kilimo, utahakikisha utekelezaji wa ajenda kuu nne za serikali unatimia.
“Kamati yangu inapigania nyongeza ya fedha zilizotengewa sekta ya kilimo ili baadhi ya marekebisho yatekelezwe na kuwanufaisha wakulima,” akasema.
Mbunge huyo pia alieleza kushangazwa kwake na uamuzi wa serikali wa kuongeza ushuru unaotozwa kwenye pembejeo za kilimo hadi asilimia 14, akisema atashauriana na Waziri Peter Munya kuhusu suala hilo.
“Serikali iliweka ushuru wa asilimia 14 kwenye pembejeo za kilimo. Hata hivyo, hili ni suala ambalo linafaa liangaziwe upya na nitakuwa nikikutana na waziri kuzungumza kuhusu ushuru huo,” akasema mbunge huyo wa Moiben.
Bw Tiren ambaye ni mwanachama wa Jubilee anayehudumu muhula wake wa pili bungeni, pia aliahidi kwamba kamati yake itashauriana na Bw Munya ili kukomesha uagizaji wa unga wa ngano kutoka nchi za nje.
Alisema unga huo umejaa sokoni na ukiendelea kuagizwa, basi wakulima wataendelea kupata hasara nyingi.Hivi majuzi, serikali ilitangaza kwamba haitakuwa ikiamua bei ya mahindi au kuyanunua, pamoja na kununua mbolea na pembejeo nyingine za kilimo.
Kuhusu hilo, Bw Tiren alisema wizara inafaa kuwaeleza wakulima kuhusu masuala hayo ili kuzuia mgongano.
“Kumekuwa na hofu kwamba wakulima hawataendelea kununua mahindi kutoka kwa wakuzaji nafaka. Nafikiri suala hili halieleweki na lazima tushirikiane na wizara kuwahamasisha wakulima kulihusu. Sidhani kwamba serikali inaweza kuzima kabisa ununuzi wa mahindi,” akasema.
“Ununuzi wa mahindi ya bei rahisi kutoka kwa baadhi ya mawakala umekuwa kosa kubwa kwa serikali. Kamati hii itashauriana na serikali kuhusu hilo ili wakulima wanufaike na kilimo chao badala ya watu wanaowalaghai fedha zao,” akaongeza.
Katika bajeti ya 2020/2021, serikali ilitengea sekta ya kilimo Sh52.1 bilioni huku ushuru ukiondolewa kwenye mauzo ya mahindi kati ya mageuzi mengine ya kuhakikisha kuna chakula cha kutosha nchini.
Wakulima kutoka eneo la Moi’s Bridge na Kaunti ya Uasin Gishu, nao walisifu hatua ya kutenga Sh3 bilioni ili kupunguza gharama ya ununuzi wa pembejeo za kilimo, hasa baada ya serikali kujiondoa kwenye wajibu wa kuwanunulia wakulima mahitaji hayo.
Kwenye bajeti vilevile, serikali ilitenga Sh3.4 bilioni ili kusaidia katika mradi wa kilimo cha unyunyiziaji wa mashamba maji kama njia ya kuongeza kiwango cha uzalishaji.