Mbunge ataka Matiang’i ajiuzulu, asema hawezi kazi
NA SHABAN MAKOKHA
MBUNGE wa Khwisero Christopher Aseka amemtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kujiuzulu kufuatia visa vingi vya utovu wa usalama Magharibi mwa nchi.
Bw Aseka amesema Dkt Matiang’i amewatelekeza wakazi wa Magharibi wanaovamiwa kuuawa, kuteswa na kupokezwa kipigo kikali na majambazi sugu pamoja na makundi ya uhalifu.
Wiki jana, kisa cha kutamausha kilitokea katika kituo cha kibiashara cha Mulwanda eneobunge hilo ambapo askari rungu wawili walivamiwa, moja akauawa huku mwengine akisalia akiwa hali mahututi hospitalini. Mlinzi aliyefariki ni Atito Ashira, 56 naye Francis Akhaya bado yupo hali mahututi hospitalini kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata kwa kukatwa kwa panga.
Bw Aseka akiwa ameandamana na Mwakilishi Wadi wa Kisa ya Kati, Geoffrey Ommatera waliwaongoza wenyeji kuwasilisha malalamishi yao katika kituo cha polisi wa utawala cha Mulwanda na kuwataka maafisa wote kituoni humo kupewa uhamisho kwa kuzembea kazini na kushindwa kuwanasa wahalifu.
Hata hivyo maandamano hayo yalikabiliwa na polisi hao waliowarushia vitoa machozi na kufyatua risasi kadhaa hewani huku Bw Aseka akishangaa iweje wahalifu walitekeleza uvamizi huo mita 20 pekee kutoka kituoni humo bila ufahamu wowote wa polisi.
Baadaye ilibainika polisi walitumia risasi halisi kuwatawanya waandamaji huku mbunge huyo akikusanya risasi hizo sokoni humo na kuahidi kuziwasilisha katika Bunge la Kitaifa ndipo aelezwe sababu ya polisi kuzitumia.
“Nataka amri itolewe ili Dkt Matiangi afike mbele ya bunge na awaeleze Wakenya kwa nini polisi wa Khwisero walitumia risasi halisi kuwakabili waandamanaji . Akikosa kufanya hivyo basi tutamsukuma hadi ajiuzulu kwa kushindwa kazi,” akasema Bw Aseka.
Akiwahutubia wenyeji baada ya kisa hicho, Kamanda Mkuu wa Polisi Kaunyi ya Kakamega Wilkister Vera aliwaonya maafisa wake wanaoshirikiana na wahalifu kwamba watachukulia hatua kali za kinidhamu.
Wabunge Alfred Agoi, Omboka Milemba na Bernard Shinali pia walimtaka Dkt Matiang’I kutembelea eneo hilo na kufariji familia waliopoiteza jamaa zao.
Hii ni baada ya tukio sawa na hilo kutokea katika soko la Kilingili, kaunti ya Vihiga na kupelekea vifo vya walinzi sita.