Mbunge ataka Uhuru na Raila wamng'oe Ruto
Na Stanley Ngotho
MBUNGE wa Kajiado ya Kati, Bw Elijah Memusi, amewarai Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuwashinikiza wabunge wanaoegemea upande wao kuwasilisha hoja ya kumng’oa mamlakani Naibu Rais William Ruto.
Bw Memusi amedai kwamba Dkt Ruto anahatarisha usalama wa kitaifa baada ya walinzi wake kupatikana nyumbani kwa Mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi alipokuwa akisakwa na polisi hivi majuzi.
Akihutubu katika mkutano eneobunge lake jana, Bw Memusi alisema kukamatwa kwa walinzi wa Dkt Ruto kumeibua maswali mengi kuhusu usalama na ni suala la kuchunguzwa mara moja.
Bw Sudi alikamatwa na kuachiliwa Ijumaa na mahakama mjini Nakuru kwa tuhuma za kutoa matamshi ya uchochezi.
“Ningetaka kumwambia Rais Kenyatta kwamba, ikiwa naibu wake amekuwa kikwazo, anapaswa kuungana na Bw Odinga na kiongozi wa KANU, Gideon Moi kuwaunganisha wabunge wao kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Dkt Ruto,” akasema.