Mbunge hatarini kupoteza kiti kwa kupigia Ruto debe
Na RUTH MBULA
WAKAZI wa Mugirango Kusini huenda wakarejelea uchanguzi wa ubuge iwapo maagizo yaliyotolewa na chama cha Kenya National Congress (KNC) kwa msajili wa vyama vya kisiasa ili kumuondoa Bw Sylvanus Osoro, yatafaulu.
Chama cha KNC kimwemwagiza msajili wa vyama vya kisiasa kuhusu jambo hilo baada ya mazungumzo na baraza kuu la chama hicho. Chama hicho kimetishia kumwondoa mamlakani Bw Soro kufuatia madai kuwa amefeli kutii sheria za chama.
Baadhi ya makosa yanayomwandama ni pamoja na kukosa kumwelekeza karani wa bunge la kitaifa kukata ada ya kila mwezi kwa chama hicho kama ilivyo majukumu yake kwenye chama.
Mbunge huyo anasemekana pia amekuwa akipigia debe chama kingine na pia kukosa kufika kwenye shughuli za chama chake kila mara anapohitajika kufanya hivyo. Mojawapo ya barua zilizotiwa sahihi na katibu mkuu wa chama cha KNC, Bw James Ogembo ilisoma kuwa, “Tunaelekeza ofisi yake kuondoa jina la Sylvanus osoro kutoka kwenye sajili ya chama cha KNC ambaye ni mwanachama nambari KNCKS1000077.”
Uamuzi huo wa kuomwondoa mamlakani mbuge huyo ni pigo kubwa kwani ameonekana mara kwa mara akimpigia debe Naibu wa Rais William Ruto. Mnamo Ijumaa, wakati wa mazishi ya aliyekuwa waziri msaidizi Hezron Manduku katika kijiji cha Nyaturago, Nyaribari Masaba, mbuge huyo alisikika akimpigia debe Dkt Ruto.