Mbunge wa Jomvu awaondolea wakazi hofu
Na WINNIE ATIENO
MBUNGE wa Jomvu Badi Twalib amewahakikishia wakazi wa eneobunge lake kwamba madereva wa masafa marefu hawatapimwa virusi vya corona katika kituo cha afya kilichoko Miritini.
Aidha hapo Jumapili, serikali kuu iliagiza madereva wote kupimwa katika kituo cha afya cha Miritini.
Hata hivyo, Bw Twalib alisema katika mashauriano na serikali ya kaunti ya Mombasa, agizo hilo lilifutiliwa mbali kutokana na hatari iliyopo.
Bw Twalib alisitiza kuwa madereva hao watapimwa katika sehemu mbadala ambapo hakuna wananchi wengi.
Akiongea na wanahabari huko Jomvu, Bw Twalib aliwataka wamiliki wa kampuni za usafiri kushirikiana na serikali ya kaunti ili kutekeleza mchakato wa kupima madereva wao kwenye kampuni hizo.
“Kuwapima madereva dhidi ya virusi vya Covid-19 kwenye hospitali ambayo iko katika sehemu ya makazi ni hatari sana kwa umma. Hii itahatarisha wakazi na kuwaweka katika hatari ya maambukizi; badala yake wanafaa kupimwa katika kampuni zao,” alisema.
Aliongeza kuwa waendeshaji bodaboda pia watawekwa katika hatari watakapokuwa wakiwasafirisha madereva hao hadi katika hospitali hiyo.
Bw Twalib aliwahakikishia wakazi kwamba swala hilo limetatuliwa.
Hata hivyo, aliwasihi kuendelea kufuata maagizo ya Wizara ya Afya ikiwemo kuvaa barakoa, kuosha mikono na kukaa nyumbani.
“Taharuki ilitanda pindi serikali kuu ilipowaagiza madereva kupimwa virusi vya corona katika hospitali hii ambayo iko katika sehemu ya makazi ambapo njia ya kuingia na kutoka ni moja. Lakini swala hilo limetatuliwa na hiyo hospitali ilifungwa kufuatia ukosefu wa madaktari,” alisitiza.
Bw Twalib alisema kampuni nyingi zilizoko eneo hilo zina zaidi ya madereva 300.