• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Mbunge wa zamani adaiwa kodi ya miezi mitano

Mbunge wa zamani adaiwa kodi ya miezi mitano

Na BRIAN OCHARO

MAHAKAMA ya Watoto mjini Mombasa imeamuru aliyekuwa mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa alipe deni la kodi ya Sh140,000 ili kuzuia kufukuzwa kwa familia yake kutoka makazi yao eneo la Nyali.

Agizo hilo lilitolewa baada ya Rehema Susan Maalim ambaye anadai kuwa mke wa Bw Ndegwa, kuiambia mahakama kuwa mshtakiwa huyo amekwepa majukumu na kumwachia malezi kwa miezi mitano iliyopita.

Mahakama ya Watoto ya Tononoka ilimuamuru Bw Ndegwa alipe deni hilo la miezi mitano, ili mwanamke huyo na mtoto wake wasifurushwe kutoka makazi hayo.

“Bw Ndegwa ameamriwa kulipa deni la kodi ya nyumba ambayo inahitajika na mwenye nyumba huku kesi hii ikisubiri kusikizwa na kuamuliwa,” Hakimu Mkuu Mkazi, Bi Lucy Sindani alisema.

Mwanamke huyo aliiambia mahakama kwamba Bw Ndegwa ambaye amekuwa akilipia nyumba hiyo amedinda kuwajibikia majukumu yake kwa muda wa miezi mitano na kwamba madalali wametishia kumfukuza na kuuza mali yake ili kulipia deni ambalo anadaiwa .

Bi Maalim alitaja jambo hilo kama la dharura n kuomba mahakama kuingilia kati haraka huku akisema yeye na binti yake watapoteza makao kama mshtakiwa hatalazimishwa kulipa deni hilo.

Mwanamke huyo alisema katika malalamiko yake mbele ya mahakama kwamba alikutana na Bw Ndegwa mwaka wa 2014 huko Lamu, ambako walipendana na kisha baadaye wakazaa mtoto mmoja.

“Mimi na mshtakiwa hapo awali tulikuwa wenyeji wa Lamu ambapo tulikutana lakini mwaka 2017, nilihamia Mombasa ambako nilianza biashara,” alisema.

Mwanamke huyo anaelezea kwamba alipohamia Mombasa, alikodisha nyumba eneo la Mkomani ambako alikuwa akilipa Sh18,000 kila mwezi, lakini wakati Bw Ndegwa alimtembelea, alimuamuru atafute nyumba nzuri zaidi kwani hakuifurahia.

Bi Maalim alisema kuwa Bw Ndegwa alimpeleka kwenye ghorofa eneo la Nyali ambako amekuwa akilipa kodi ya Sh35,000 kila mwezi, akiongeza kuwa mstakiwa pia alimuongezea vitu vya nyumba.

“Wakati alipotutembelea Februari mwaka jana, hakuvutiwa na nyumba akisema msichana wake hawezi kuishi katika nyumba kama hiyo. Alituhamisha hadi maghorofani na tangu wakati huo amekuwa akilipa kodi,” alisema katika ithibati yake.

Bi Maalim pia alisema kando na mshtakiwa kulipa kodi, alikuwa akituma Sh40,000 kila mwezi za matumizi ya mtoto na gharama nyingine.

Mwanamke huyo aliiambia mahakama kuwa mambo yalianza kuenda mrama mwaka jana Novemba wakati Bw Ndegwa aliacha ghafla kulipa kodi na kutuma fedha za matumizi.

Mwanamke huyo alisema Bw Ndegwa ni mbunge wa zamani, mfanyabiashara na kwa sasa mwanachama wa bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Pwani na kuwa anaweza kukidhi mahitaji ya mtoto wake lakini ameamua kukwepa wajibu.

“Ni kwa manufaa ya mtoto ndipo ninasihi mahakama iruhusu ombi langu la kumlazimisha Bw Ndegwa kutimiza majukumu yake,” alisema.

Bw Ndegwa hata hivyo hajajibu madai ya mlalamishi huyo licha ya mahakama kuonya kwamba iwapo hatafika mahakamani, kesi hiyo itasikizwa na kuamuliwa bila yeye.

You can share this post!

Uhuru aungana na familia ya mzee Moi kuomboleza

Mbosso avunja nyoyo za mashabiki sababu ya malipo

adminleo