Habari Mseto

Mbunge wa zamani kujibu shataka Desemba 1

November 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Mutuku alimwamuru aliyekuwa Mbunge wa Tetu James Ndung’u Gethenji afike kortini mwezi ujao kujibu shtaka la kughushi stakabadhi za uthibiti wa mali ya baba yao iliyo na thamani ya Sh20bn.

Bi Mutuku alimwagiza Bw Gethenji afike mbele yake Desemba 1,2020 kujibu shtaka la kughushi hati alizompelekea msajili wa masuala ya makampuni katika afisi ya mwanasheria mkuu mnamo November 18 2018.

Kwa mujibu wa shtaka lililowasilishwa mbele ya Bi Mutuku, Bw Gethenji alighushi  arifa za mkutano mkuu wa kampuni ya Kihingo Village Waridi Garden Management One Limited inayomiliki nyumba za kifahari zilizoko mtaani Kitsuru jijini Nairobi.

Wakili Ishmael Nyaribo anayemwakilisha Bw Gethenji aomba afike kortini Desemba 1,2020. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Hakimu alitoa agizo Bw Gethenji afike kortini Desemba 1,2020 baada ya kuelezwa ni mawakili Ishmael Nyaribo, Nelson Osiemo na Willis Otieno kwamba “mshtakiwa hawezi kufika kortini kwa vile yuko karantini baada ya mmoja wa watu wa familia yake kuambukizwa ugonjwa wa Corona.”

Kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda hakupinga ombi hilo.

Bw Gikunda aliomba dhamana ya Sh20,000 ya polisi aliyopewa mwanasiasa huyo itumike hadi atakapofika kortini.

“Hii mahakama imekubalia ombi la Bw Gethenji akubaliwe kufika kortini Desemba 1,2020,” alisema Bi Mutuku.