MCAs watishia kufufua hoja ya kumtimua Sonko
COLLINS OMULO na VALENTINE OBARA
MADIWANI wa Kaunti ya Nairobi wametishia kufufua hoja ya kumng’oa mamlakani Gavana Mike Sonko.
Madiwani hao walimlaumu Bw Sonko kwa kuanza upya vioja jijini, kuhangaisha shughuli za Idara ya Huduma za Nairobi (NMS) iliyo chini ya afisi ya rais, na wakadai anatatiza pia shughuli za bunge la kaunti kupitia kwa wandani wake.
Hivi majuzi, gavana huyo alianzisha ziara mashinani kwa lengo la kuonyesha umma kwamba, kuna miradi aliyoanzisha, akihofia sifa zote zitaenda kwa NMS inayosimamiwa na Jenerali Mohamed Badi.
Mwishoni mwa wiki, alidai hakujua kile alichotia sahihi Ikuluni kwa vile alikuwa amenyweshwa pombe.
“Rais alikuwa amemwokoa asitimuliwe. Tulishuhudia akishindwa kutekeleza wajibu wake akakabidhi majukumu muhimu ya kaunti kwa serikali kuu. Anamkosea heshima Rais akidai alitia sahihi stakabadhi hizo akiwa mlevi Ikuluni. Anajaribu kusema Ikulu ni kiwanda cha pombe?” wakashangaa madiwani hao, katika taarifa ya pamoja.
Diwani wa Embakasi, Bw Michael Ogada, alisema watakapoanza upya mchakato wa kumtimua Sonko, serikali kuu isiingilie kati.
Huku akimhusisha gavana huyo na masaibu yanayomkumba Spika wa Bunge la Kaunti Beatrice Elachi, ambaye ametishiwa kung’atuliwa na baadhi ya madiwani, alisema viongozi wakuu wanafaa kuwaacha madiwani wafanye kazi yao hoja hiyo itakapofufuliwa.
“Hatutaki tuitwe tena tuambiwe tusimtimue Sonko. Badala ya kumtimua Elachi, kutakuwa na tukio jingine kwani shughuli yetu itakuwa ni kumfurusha Sonko,” akasema.
Bi Elachi alihusisha masaibu yake mapya na uamuzi wa kumwondoa karani wa kaunti Jacob Ngwele, ambaye ni mwandani wa Sonko, na pia kwa kuunga mkono NMS.
“Amejua sasa kwa vile Ngwele hayupo tena, kuna uwezekano atatimuliwa,” akasema.
Hata hivyo, msemaji wa gavana huyo, Bw Ben Mulwa, alisema Bw Sonko hahusiki kivyovyote na mipango ya kumng’oa spika mamlakani.
Bw Mulwa pia alipuuzilia mbali juhudi mpya za kutaka kumtimua gavana huyo, akisema kuna maswala muhimu kuhusu usimamizi wa kaunti ambayo madiwani wanafaa kujibu badala ya hilo.