Mchakato wa kumng’oa Jaji Maraga waanza
Na BENSON MATHEKA
WAKILI mmoja wa Nairobi, amewasilisha ombi bungeni akitaka Jaji Mkuu David Maraga na makamishna saba wa Tume ya Huduma kwa Mahakama (JSC) waondolewe.
Katika ombi hilo, wakili Adrian Njenga anataka bunge kuwaondoa makamishna hao kwa kile anachotaja kuwa na tabia isiyofaa. Bw Njenga amewataja Bw Maraga, naibu wake Philomena Mwilu, Jaji Mohammed Warsame, Jaji Aggrey Muchelule, wakili Tom Ojienda, Bi Emily Ominde na Bi Mercy Deche katika ombi lake kwa bunge.
Wakili huyo anawalaumu makamishna hao wanaowakilisha vitengo tofauti vya mahakama na chama cha mawakili (LSK) kwa kukiuka Katiba.
“Wameshindwa kulinda na kufanikisha uhuru na uwajibikaji katika Mahakama na uwazi katika utoaji wa haki,” anaeleza katika ombi lake.
JSC ina makamishna kumi na wawili. Mbali na anaotaka waondolewe, wengine ni walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta ambao walihojiwa na bunge wiki jana.
Wao ni Profesa Olive Mugenda, Bw Patrick Gichohi na Bw Felix Koskei. Mwanasheria Mkuu pia huwa kamishna wa tume hiyo inayoajiri majaji, mahakimu na maafisa wengine wa mahakama. Msajili wa Mahakama Anne Amadi ni katibu wa tume hiyo.
Bw Njenga analaumu makamishna aliotaja kwa kuwalinda, kuwatetea na kuwaondolea lawama majaji anaodai wanahusika na tabia isiyofaa. “Wamepuuza, bila kuzingatia Katiba, malalamishi yanayowasilishwa katika JSC,” wakili huyo anasema kuhusu makamishna hao.
Ombi hili linaonekana kama juhudi za serikali za kuingilia uhuru wa mahakama ambayo inadai inatatiza shughuli zake.
Itakumbukwa kuwa Mahakama ya Juu ilipobatilisha ushindi wa Uhuru Kenyatta, Rais aliahidi kuchukulia mahakama hatua akishinda uchaguzi wa marudio na kuwataja majaji kuwa wakora.
JSC ni muhimu katika kuleta mabadiliko katika mahakama kwa sababu inaajiri majaji, kupokea na kushughulikia malalamishi kuhusu maafisa wa mahakama.
Tume hiyo ina nguvu za kutoa mapendekezo kwa Rais kuunda jopo la uchunguzi ikipata kwamba kuna sababu za kumuadhibu jaji.Hata hivyo, kumuondoa Jaji Mkuu kitakuwa kibarua kikuu kwa sababu itabidi sheria ya JSC ibadilishwe au wafutwe kazi.
Mwaka jana, mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu aliwasilisha ombi kwa JSC akitaka Bw Maraga na naibu wake Mwilu waondolewe ofisini.