Habari Mseto

Melly asafisha kozi zinazodaiwa kuwa 'feki'

February 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CAROLYNE AGOSA

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu na Utafiti Bw Julius Melly, amepuuzilia ripoti ya hivi majuzi kwamba kozi 133 zinazofunzwa katika baadhi ya vyuo vikuu humu nchini ni feki.

Kulingana na ripoti hiyo, wanafunzi zaidi ya 10,000 wanaosomea kozi za digrii katika vyuo vikuu 26 wako hatarini kupokezwa vyeti ‘feki’ kwa sababu kozi hizo sio halali.

Ripoti hiyo ya Ofisi ya Kutoa Nafasi za Vyuo Vikuu na Vyuo Kenya (KUCCPS) inasema kuwa Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) haijaidhinisha kozi hizo na hivyo ni feki.

Hata hivyo, Bw Melly amewahakikishia wanafunzi husika kwamba kozi sio feki.

“Hakuna kozi yoyote inayofunzwa hapa nchini bila kuidhinishwa na mamlaka husika,” akasema katika kongamano la Kamati ya Bunge kuhusu Elimu na wadau wa elimu ya juu mjini Nairobi lililokamilika Ijumaa.

Madarasa

Bw Melly pia alitoa wito kwa shule za upili na vyuo vikuu kujenga madarasa zaidi ili kupokea wanafunzi wa ziada wanaojiunga na taasisi hizo kutokana na mpango wa serikali wa kuhakikisha wanafunzi wote wanaofanya mitihani ya kitaifa wanasonga mbele katika elimu yao.

Hata hivyo, wito huo utakumbwa na changamoto ilizingatiwa kuwa serikali ndiyo hufadhili shule za umma. Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wakuu wa shule kuhusu kucheleweshwa kwa fedha hizo.