Habari Mseto

Mfumo wa kidijitali bungeni kurahisisha huduma

May 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Hatua ya Bunge ya kuzindua mfumo wa kidijitali katika operesheni zake itaokoa wananchi mamilioni kila mwaka.

Hii ni kwa mujibu wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ambayo imesema kuwa mfumo wa kidijitali umerahisisha operesheni zake, kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake na kuongeza kasi ya utekelezaji kutokana na kuwa wabunge wanaweza kupata stakabadhi zote kwa iPad.

“Hatua hiyo imeongeza kiwango cha uwazi, imekuwa rahisi kupata stakabadhi kama vile miswada na maagizo. Imekuwa rahisi zaidi kupata habari ambayo kwa kawaida inaweza kuchukua muda mrefu kupata,” alisema afisa wa PSC.

Ni rahisi sasa kwa wabunge na maseneta kupata habari zozote kuhusiana na operesheni za bunge kupitia mfumo huo.

Karani wa Bunge Michael Sialai April alisema mfumo wa dijitali ungehifadhia serikali Sh15 milioni kila mwaka kutokana na kuwa hakuna kuchapishwa kwa habari, miswada na maagizo.

“Tutahifadhi zaidi kwa kutangamanisha mfumo wote na kuutumia kuweka habari zote za Bunge,” alisema Sialai.

Uzinduzi wa mfumo huo ulifanywa katika sehemu tatu ambapo maafisa wa habari, mawasiliano na teknolojia wa Bunge la Kitaifa na Seneti walipewa mafunzo.

Sehemu ya pili ilihusu kutoa mafunzi kwa makarani, maafisa wa utaratibu na maafisa wote ambao hufuatilia muhimu.

PSC ilinunua iPad 350 kwa matumizi ya wabunge na zingine 71 kwa matumizi ya maseneta.