Mganga amchemsha mtoto mchanga na kumuua akidai ni tiba
Na GERALD BWISA
POLISI mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia wamemkamata daktari wa kienyeji ambaye anatuhumiwa kumuua mtoto wa mwaka mmoja, baada ya kumtia ndani ya maji ya kuchemka ili kumponya ugonjwa wa cerebral palsy ambao husababisha matatizo ya kiakili.
Kamanda wa Polisi wa kaunti hiyo, Bw Ayub Ali alithibitisha wanamzuilia mganga huyo, Millicent Akinyi, 22, anayetoka eneo la Tuwan, huku uchunguzi kuhusu kifo cha mtoto huyo ukiendelea.
“Tulimkamata na tukamfikisha kortini. Korti ilituruhusu kumzuilia kwa siku 14 ili tukamilishe uchunguzi,” Bw Ali akasema.
Kulingana naye, daktari huyo alichemsha maji yakatokota, akatia chumvi na dawa za kienyeji kisha akamtumbukiza mtoto ndani, akidai alikuwa akimponya.
Alisema mtoto huyo alianza kulia lakini daktari huyo akamhakikishia mamake kuwa kilio kilikuwa ishara ya mapepo kuondolewa kutoka ndani ya mtoto.
“Alipomtoa mtoto kutoka ndani ya maji, tayari ngozi ilikuwa imebambuka tumboni ndipo mamake mtoto akatoka ndani ya nyumba hiyo akilia,” akasema Bw Ali.
Ni majirani ambao walikimbia katika boma hilo na kumchukua mtoto kisha wakamkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kitale kwa matibabu.
Alilazwa katika hospitali hiyo lakini baada ya siku mbili akazidiwa na maumivu na kukata roho.
Wakati Taifa Leo ilizuru mtaa wa Kisumu Ndogo ambapo familia hiyo inaishi, hali ya huzuni ilikuwa imetanda, mamake mtoto huyo, Bi Judy Gideon akiwa bado hajaamini hali iliyomkumba.
Alisema mtoto wake ambaye alimzaa Februari mwaka uliopita kwa njia ya upasuaji alikuwa sawa, hadi alipohitimisha miezi miwili ambapo alianza kupata matatizo ya kiafya kwa kudhoofika shingoni na mguu wake wa kulia.
“Hakuwa akisimama kwa uthabiti na nilipomsimamisha alikuwa akianguka,” akasema Bi Judy, na kuongeza mtoto wakati fulani alikuwa mkavu na kutetemeka.
Ni hapo ambapo alifahamishwa kuhusu daktari wa kienyeji na majirani, ambaye angemsaidia kusuluhisha shida yake, baada yake kumpeleka mwanawe katika hospitali ya rufaa ya Kitale bila mafanikio.
Jumatatu wiki iliyopita, mama huyo alimpeleka mwanawe kwa daktari huyo wakiwa pamoja na mwanamke mwingine, ambaye naye alikuwa ameenda kutafuta suluhu ya ndoa yake, kutokana na hali ya mumewe kuwa na jicho la nje.
“Tulipofika nyumbani kwa daktari huyo wa kienyeji, tulimpata akiwa amechemsha maji na akayatoa motoni. Alitia chumvi, akaongeza dawa nyingine na akaniagiza nimpe mtoto ili amtibu. Nilimpa mtoto na mara moja akamtia katika maji, ambayo yalikuwa yamechemka. Mtoto aliungua vibaya,” akasema mama huyo.
Jirani ya daktari huyo kwa jina Francisca Erokodi alisema kuwa amekuwa akiuza dawa za kienyeji na kudai kuwa ana uwezo wa kuponya magonjwa tofauti kwa dawa hizo.
“Nimekuwa nikiona watu wakiingia katika nyumba yake na kuongoka tangu alipokuja eneo hili,” akasema.
Lakini mwanaharakati wa kutetea masuala ya jinsia Tuwan Edward Omondi alilaani kitendo hicho na akawataka wanawake kupeleka wanao hospitalini wanapokuwa wagonjwa.