Mgeni atoroka na mtoto katika hali ya kutatanisha
Na MARY WAMBUI
FAMILIA moja inaendelea kuhangaika baada ya mwanamke aliyekuwa amemtembelea jirani wao kutoweka na mtoto wao wa miezi mitano katika kisa cha kutatanisha mtaani Utawala, katika Kaunti ya Nairobi.
Pauline Ilenje, 24, ambaye ni mamake mtoto huyo Harold Ochieng’ alikuwa akifanya kazi nyumbani akiwa amemfungia mwanawe akilia mgongoni.
Hapo ndipo mwanamke mgeni kutoka nyumba ya jirani alimwonea huruma na akamwomba amkabidhi mtoto huyo ambebee hadi amalize kazi aliyokuwa akifanya.
“Aliniomba anibebee mtoto hadi nimalize kazi niliyokuwa nikifanya na nikakubali,” akasema Bi Ilenje.
Kile ambacho hakufahamu ni kwamba mwanamke huyo kwa jina Aisha hakuwa na nia nzuri na alikuwa akipanga njama ya kutoroka na mwanawe.
Baada ya kumaliza kazi zake za nyumbani, Bi Ilenje alianza kumtafuta mwanawe kwenye nyumba ya jiraniye na maeneo ya karibu lakini hakumpata. Kumbe mwanamke yule alikuwa ashatoroka naye, jambo ambalo lilimsababishia wasiwasi na mahangaiko makubwa hadi leo.
Bi Ilenje alimpigia mumewe David Ochieng’ mwenye umri wa miaka 43 simu lakini pia hakumpata ndipo akakimbia kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha utawala.
“Nilikimbia hadi kituo cha polisi cha utawala kupiga ripoti na maafisa hao wakaniagiza nirejee na jirani yangu kituoni,” akasema.
Bw Ochieng’ baadaye saa saba mchana alifika nyumbani na kuungana na mkewe kumtafuta mwana wao huku pia akimpigia simu jiraniye na kumuuliza kuhusu alikokuwa mgeni wake.
Walikumbana na jirani yake saa kumi akiondoka akionekana kuwa na haraka ndipo wakaelekea naye katika kituo cha Utawala ili ahojiwe. Jirani huyo pia alidai kwamba Bi Aisha alikuwa tu mfanyakazi aliyemwita kumsaidia kazi za nyumbani wala hakuwa na ukoo au uhusiano naye.
“Maafisa hao walituambia tutafute nyumba ya Aisha na tukaipata Githunguri katika Kaunti ya Kiambu. Hata hivyo, hatukumpata japo mlango ulikuwa wazi na hakukuwa na mtu ndani. Majirani wake walituambia walimwona akiondoka akiwa na mtoto na begi,” akasema Bw Ochieng’.
Baadaye polisi katika kituo cha utawala waliwaambia wapige ripoti katika kituo cha polisi cha Ruai kisha waendelee kumtafuta mwanao. Walirejea Githunguri kwa matumaini kwamba wangempata Bi Aisha lakini nyumba yake bado haikuwa na mtu.
Walimpata mtoto mdogo aliyewaarifu kwamba mwanamke huyo alikuwa akiishi hapo ila hakuwa amerejea.
Polisi kutoka kituo cha polisi cha Ruai walikataa kuzungumzia kisa hicho japo wanandoa hao walisema walielezwa maafisa hao walikuwa wakiendelea kufuatilia simu ya Bi Aisha ili kufahamu aliko na mtoto huyo.