Mgogoro waibuka kufuatia kifo cha mwanamke aliyefariki akifanyiwa upasuaji wa urembo
HOSPITALI inayofanyia wanawake upasuaji ili kuwarembesha, imepeleka kesi mahakama kuu kupinga hatua ya baraza la madakatari nchini (KMPDC) kuifunga baada ya mwanamke kuaga dunia.
Aghalabu wanawake hufanyiwa upasuaji kuunda sehemu ya tumbo na makalio.
Omnicare Medical imewasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga hatua ya KMPDC kutoa amri ifungwe baada ya kufariki kwa mwanamke huyo.
Mhasiriwa alilazwa hospitalini humo kufanyiwa upasuaji wa kurembeshwa kisha akaaga dunia siku 10 baadaye katika hospitali tofauti.
Omnicare inadai hatua ya KMPDC kutaka ifungwe inakiuka haki zake za Kikatiba kuendeleza huduma kwa wateja wake.
Hospitali hiyo imefichua kwamba imeajiri madaktari waliohitimu na kwamba mhasiriwa alifia katika hospitali nyingine.
Katika kesi iliyoshtakiwa na wakili Danstan Omari, Omnicare imeeleza bayana kwamba mteja huyo alifika mle Oktoba 16,2024 akitaka afanyiwe upasuaji wa kurembeshwa ujulikanao kwa lugha ya utalaamu Liposuction.
Bw Omari ameeleza katika utaratibu huo madaktari huchuna mafuta kutoka sehemu moja ya mwili na kupachika sehemu nyingine.
Sehemu ambazo huchunwa nyama na mafuta ni kwenye tumbo, makalio, mapajani, mikono ama shingoni.
Kufuatia utaratibu huu, sehemu inayopachikwa mafuta haya urembeka mno na kuchukua urembo asili. Wanawake wengi hufanyiwa upasuaji kuunda makalio.
Katika kesi iliyowasishwa na Bw Omari, Omnicare imedai ilimfanyia mteja wake upasuaji huo baada ya kumfanyia vipimo mbalimbali.
Pia mwanamke huyo alikuwa amefanyiwa ukaguzi katika hospitali nyingine iliyo na tajriba ya juu katika taaluma ya tiba iliyoko jijini Nairobi.
Mnamo Oktoba 16, 2024 Omnicare ilimfanyia upasuaji mwanamke huyo.
Alitarajiwa kutoka hospitali mnamo Oktoba 17 kisha akaomba akae hadi Oktoba 18,2024.
Kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani, mwanamke huyo alilalamika alikuwa anaumwa na kifua.
Alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani lakini mnamo Oktoba 26,2024 katika hospitali nyingine.
Hospitali hiyo imeeleza kwamba mnamo Oktoba 29, 2024 mhasiriwa alifanyiwa upasuaji.
Daktari wake alihudhuria hafla hiyo ya upasuaji na ripoti kuhusu kilichosababisha kifo hicho bado haijatolewa.
Mahakama imeelezwa na Bw Omari kwamba KMPDB iliiandikia barua mnamo Oktoba 31, 2024, ikiitisha taarifa za madaktari waliofanyia upasuaji huo.
“Hospitali yetu imeajiri madaktari na wauguzi waliohitimu,” Bw Omari ameeleza katika kesi anayoomba iratibiwe kuwa ya dharura.
Kabla ya kupeleka majibu ya barua hiyo, Omnicare inadai ilivamiwa na genge la wahuni waliotisha kuiteketeza moto.
Mahakama imeelezwa kwamba iwapo haitaingilia mzozo huo, wakenya wengi walioajiriwa watakosa ajira.
Pia wakili amesimulia kwamba haki za kutoa huduma kwa wateja zitakiukwa.
Omnicare imeomba mahakama ipige marufuku amri ya kufunga hospitali hiyo.
Pia inaomba mahakama kuu iamuru inaendeleza huduma halali.
Katika kesi hiyo, Omnicare imeishtaki KMPDB, Wizara ya Afya ma Mkurugenzi wa Huduma za Afya Kaunti ya Nairobi.