Mgomo sasa watatiza huduma nyingi kaunti
Na BONIFACE MWANIKI
HUDUMA za serikali zimekwama katika Kaunti ya Kitui kufuatia mgomo wa wafanyakazi katika idara tofauti za kaunti hiyo.
Wafanyakazi hao wanalalamikia kuchelewa kulipwa mishahara yao ya mwezi Julai.
Hii si mara ya kwanza kwa kaunti ya Kitui kukumbwa na masaibu ya aina hii, kwani mwezi uliopita wa Julai, wafanyakazi hao walikuwa kwenye mgomo kufuatia kuchelewa kwa mishahara yao.
Kufuatia kuchelewa kwa mishahara yao mwezi huu, wafanyakazi hao wamekuwa wakisusia kazi kuanzia mwanzoni mwa wiki hii, na mnamo Jumanne walisitisha kabisa huduma zao, huku wagonjwa waliolazwa katika hospitali za serikali wakiachwa hoi.
Shughuli za kawaida katika hospitali za Kitui zimesimama kabisa na Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi katika kaunti ya Kitui, Bw Benjamin Munyalo, amewashauri wakazi waondoe wagonjwa wao kutoka hospitali za kaunti.
“Hakutakuwa na madaktari wa kuwahudumia hadi pale ambapo kaunti itawalipa wahudumu mishahara yao. Tunaomba kila aliye na mgonjwa wake amchukue na kutafuta tiba kwingine,” akasema Bw Munyalo.
Wafanyakazi kutoka idara tofauti za kaunti hiyo waliandamana hadi kwenye ofisi za Gavana Charity Ngilu wakitaka kujua uhakika wa mishahara yao ya Julai.
Baada ya kukosa nafasi ya kuzungumza na Bi Ngilu, wafanyakazi hao waliwataka wenzao wote kususia kazi na kuwasishi wauguzi waliobaki hospitalini kushughulikia huduma za dharura pia kuondoka.
“Hatuwezi kufanya kazi bila malipo kwani hata pia sisi tuna mahitaji yanayohitaji pesa. Ingekuwa heri serikali ya kitaifa ianze kushughulikia malipo ya wafanyikazi wa kaunti kwani magavana wamedhihirisha wazi kuwa hawawezi kulipa wafanyakazi wao kwa wakati unaofaa,” alisema Bw Munyalo.
Akizungumza kwa niama ya wafanyakazi wenzake, alisisitiza kuwa inampasa gavana Ngilu atafute mbinu mbadala za kuwalipa wafanyakazi wa Kitui kama vile kutumia ushuru unaokusanywa, jinsi inavyofanyika katika baadhi ya kaunti nchini.
“Tunaomba gavana wetu aige mfano wa kaunti ambazo zimewalipa wafanyakazi wao, badala ya kutumia kutoelewana baina ya bunge la kitaifa na lile la seneti kutugandamiza,” aliongeza katibu huyu mkuu.
Wagonjwa waumia
Nao wagonjwa katika hospitali tofauti katika kaunti hiyo, wameendelea kuumia kufuatia mgomo huo.
Shughuli za ukusanyaji ushuru katika maeneo tofauti haswa kwenye vituo vya mabasi pia zimesitishwa kutokana na mgomo huo wa wafanyakazi.
Bi Mary Ngava ambaye ni mmoja wa wagonjwa katika hospitali kuu ya kaunti hiyo mjini Kitui, alimsihi gavana wa kaunti hiyo kutafuta mwafaka baina yake na wafanyakazi, kwani wagonjwa wataendelea kuumia kwani wengi wao hawana fedha za kutafuta matibabu kwenye hospitali za kibinafsi.
“Wagonjwa wengi wanaotafuta matibabu katika hospitali za umma ni maskini, hivyo hawawezi kugharamia matibabu yao katika hospitali za kibinafsi; Iwapo huu mgomo hautasitishwa tutateseka sana,” alieleza.
Bw James Muturi ambaye mkewe pia amelazwa alieleza kuwa hana fedha za kumhamishia kwingine.