Mhispania kizimbani kwa kumlaghai Mwitaliano Sh14m
Na RICHARD MUNGUTI
MFANYABIASHARA wa kimataifa ambaye ameishi humu nchini kwa mwongo mmoja alishtakiwa Jumtatu kwa kushiriki katika biashara feki ya dhahabu.
Jean Emmanuel Morlon, raia wa Uhispania , alikanusha mashtaka mawili ya kumlaghai, mfanyabiashara mwingine wa kimataifa Bw Italiana Antonio Cianci dola za Marekani 140,000, sawa na Sh14 milioni.
Bw Morlon aliyeomba mahakama asomewe kiingereza kwa utaratibu ili aelewe barabara alikanusha mashtaka mawili alipofikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot.
“Naomba mahakama inisomee kiingereza kwa utaratibu na sio kwa kasi ndipo niyaelewe mashtaka,” Morlon alimsihi hakimu.
Mahakama ilimsomea kwa utaratibu mashtaka mawili dhidi yake ndipo “ayafahamu na kuelewa barabara.”
Hakimu alimweleza mshtakiwa kuwa katika mtaa wa Kileleshwa alikuwa ameweka mashine za kuyeyusha dhahabu na kupanga ndani ya masanduku vyuma vilivyokuwa vimefanana na dhahabu.
Alielezwa mashtaka yanasema alilangai Bw Cianca Dola za Marekani 140.000 akidai vyuma vilivyofanana na dhahabu hiyo ilikuwa ni dhahabu halisi.
Mahakama ilifahamishwa kesi dhidi ya Morlon itaunganishwa na nyingine dhidi ya Bw Kobia aliyeshtakiwa pamoja na Tanya Yvonne Goes, Simon Kang’ara Wainaina, Paul Gichuhi, Benjamin Mutisya, Patrick Ngula Maweu, Samson Kibet Sirkoi,Faith Kioko, Joyce Waeni, Miriam Nyambura, Consolata Thirindi Iburi,James Masai,Kathambi na Gabriel Ndururi Murage.
Wote 15 wanakabiliwa na shtaka la kufanya njama za kulaghai.
Walidaiwa kati ya Aprili 23 na 25 2019 katika eneo la Riverside mtaani Kileleshwa walifanya njama za kumlaghai Italiano Antonio Cianci , mkurugenzi wa kampuni ya Iron & Steel DMC DMCC yenye makao yake mjini Dubai Dola za Marekani 140,000 (Sh14 milioni).
Washukiwa hao wanadaiwa walikuwa wamepanga kwenye masanduku fito za dhahabu kwenye masanduku ya vyuma katika afisi za kampuni yao ijulikanayo Duaf International na pia Malca Amit Limited.
Kobia na Tanya walishtakiwa kwa kumlaghai Bw Cianci, mkurugenzi wa Iron & Steel DMCC Dola za Marekani 140,000 (Sh14milioni) wakimdanganya walikuwa na dhahabu ya kumuuzia mnamo Aprili 25,2019.
Kesi itasikizwa Septemba 2, 2019. Wote tena 14 walishtakiwa kwa kosa la kupatikana na mitambo ya kuyeyushia dhahabu katika kampuni yao Duaf International Limited & Malca Amit Limited.
Kobia alikabiliwa na mashtaka mengine tisa peke yake ya kupatikana na mihuri na stempu za afisi ya Rais, Benki kuu ya Kenya (CBK), Muhuri wa Hakimu mkuu, muhuri wa hazina kuu ya kitaifa, muhuri wa mamlaka ya ushuru nchini, idara ya madini na msajili wa kampuni.
Bi Mutuku aliwaachilia washtakiwa kwa dhamana. Bw Kobia alipewa dhamana ya pesa tasilimu Sh2milioni, Tanya Sh1 milioni pesa tasilimu na washukiwa wengine 11 ambao ni wafanyakazi wa Kobia wakapewa dhamana ya Sh100,000 kila mmoja.