Microsoft kujenga kituo cha teknolojia Kenya
Na PETER MBURU
Kampuni ya teknolojia ya kutoka Amerika Microsoft imesema kuwa itajenga kituo cha kustawisha masuala ya teknolojia nchini, ambacho kitatoa huduma kwa mataifa ya Afrika Mashariki.
Kampuni hiyo imesema kuwa ujenzi wa kituo hicho Jijini Nairobi utatoa ajira kwa wahandisi 100 nchini, kando na kustawisha masuala ya kiteknolojia nchini na mataifa jirani.
Maafisa wakuu wa kampuni hiyo Jumatatu walizuru Ikulu ya Nairobi ambapo walikutana na Rais Uhuru Kenyatta, kuahidi kuwa kituo hicho, cha saba cha aina yake duniani kitapanua biashara na kuifanya kampuni hiyo kuwekeza eneo hili zaidi.
Maafisa hao waliongozwa na Makamu wa Rais anayehusika na michezo ya kompiuta katika kampuni hiyo Phil Spencer walipokutana na Rais.
Rais Kenyatta alifurahia na kupokea hatua ya kampuni hiyo, akisema serikali itaiunga mkono.
“Nataka ushirika huu uwe wazi na unaofaidi kampuni ya Microsoft na Wakenya. Tunataka muifanye Kenya kuwa makao yenu ya pili,” Rais Kenyatta akasema.
Kulingana Microsoft, Kituo hicho kitakuwa maalum kwa shughuli za uhandisi za kampuni hiyo ya teknolijia na washirika wake barani.
Kituo hicho aidha kitatumia utofauti wa mazingira ya kidesturi ya kanda hii ili kubuni vipawa na ujuzi wa kiwango cha juu kuleta suluhisho bunifu zinazoweza kuleta manufaa, ikasema kampuni hiyo.
Mbali na Nairobi, nchi ya Nigeria pia itakanufaika na kituo sawa na hicho, ambacho kitahudumia Afrika Magharibi.
“Vituo vya ustawishaji barani Afrika vitachangia maslahi ya kampuni ya Microsoft katika biashara zao ulimwenguni kama vile Office, Azure, na Windows kati ya zingine,” akasema Bw Spencer.
Rais Kenyatta alitumia fursa hiyo kutetea kuwa kampuni hiyo itahakikisha kuwa ubunifu wa Wakenya hauporwi.
“Hakikisheni hatutapoteza haki milki ya uvumbuzi inamilikiwa na vijana wetu. Tunahitaji ushirikiano wa uwajibikaji na uwazi,” akasema.