• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Miili ya wafu isiyo na wenyewe yatatiza hospitali ya Thika Level 5

Miili ya wafu isiyo na wenyewe yatatiza hospitali ya Thika Level 5

Na Mary Wambui

WASIMAMIZI wa Hospitali ya Thika Level Five wameeleza wasiwasi wao kuhusu idadi kubwa ya miili ya wafu ambayo jamaa za waliofariki hawajulikani katika hifadhi ya maiti ya General Kago.

Ilisemekana idadi kubwa miongoni mwa miili hiyo ni ya watu waliohusika katika ajali na waliouawa kwenye uhalifu kisha ikapelekwa hapo na polisi.

Kwa sasa kuna miili 70 isiyofahamika jamaa zao katika chumba hicho kinachoweza kuhifadhi miili 114, na mingine imekaa hapo tangu mwaka wa 2014.

“Miili hiyo inapotezea hifadhi ya maiti mapato kwani imewekwa katika nafasi ambazo zingekodishwa. Inapozidi kukaa katika chumba hicho, hospitali inazidi kutumia fedha kuiihifadhi kwa miaka hiyo yote na hali hii inatumalizia rasilimali,” akasema afisa mkuu wa afya katika Kaunti ya Kiambu, Bw Jacob Toro.

Hospitali hiyo sasa imetoa wito kwa familia ambazo jamaa zao walitoweka, kwenda katika hifadhi hiyo ili wabainishe kama jamaa zao ni miongoni mwa wale ambao miili yao imehifadhiwa huko.

Hivi majuzi, Serikali ya Kaunti ya Kiambu ilitoa wito sawa na huo kupitia kwa vituo vya redio vya Kikuyi lakini baadaye ni familia moja pekee iliyotambua mwanao ambaye alifariki katika ajali iliyotokea Githurai mwaka wa 2016.

Hata hivyo familia hiyo haingeweza kugharamia ada za uhifadhi kabla kukabidhiwa mwili huo, hali iliyolazimisha hospitali kuwapunguzia ada kutoka zaidi ya Sh300,000 hadi Sh10,000.

You can share this post!

Tikiti: ODM sasa yatishia kuadhibu Gavana Obado kwa kupinga...

Serikali ndiyo chanzo cha migomo shuleni – KUPPET

adminleo