Mikahawa sasa inauza pombe – Serikali
Na SAMMY WAWERU
Serikali Jumatatu imefichua kuwa wamiliki wa mikahawa sasa wamebadilisha biashara na kuanza kuuza mvinyo bila leseni.
Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman ametoa onyo kali kwa wanaoendesha biashara hiyo, akisema uchunguzi umeanzishwa na wahusika wataadhibiwa kisheria.
“Tumefikiwa na taarifa kuna mabaa yanayohudumu, isitoshe wakati wa utekelezaji saa za kafyu. Baadhi yao ni mikahawa inayotumia leseni ya mkahawa kuendesha biashara ya uuzaji wa pombe. Ifahamike wazi mabaa na vituo vya burudani yangali yamefungwa,” akasema.
“Inashangaza kuona maeneo ya kula yakigeuzwa kuwa mabaa. Uchunguzi unaendeshwa na wahusika watachukuliwa hatua kisheria,” alisema.
Kauli ya Dkt Aman imejiri siku moja baada ya seneta wa Nairobi Johnson Sakaja kukamatwa na maafisa wa polisi japo aliachiliwa, baada ya kupatikana akibugia pombe na watu kadhaa katika baa moja jijini Niarobi.
Kukamatwa kwa Sakaja kulifichuka kupitia video iliyosambaa mitandaoni, akionekana kufungiwa katika kituo cha polisi cha Kilimani, Nairobi baada ya kutiwa nguvuni.
Hata ingawa alikuwa amekanusha madai hayo, Jumatatu aliyakubali huku akiomba Wakenya msamaha kwa kukiuka sheria zilizowekwa kusaidia kudhibiti msambao wa Covid-19 kama kiongozi.
“Ni jambo la kusikitisha visa vinapozidi kuongezeka nayo mabaa yanaendelea kufunguliwa. Mengi ni mikahawa, na yatafungwa kwa kukiuka sheria,” akaonya Dkt Francis Kuria kutoka Wizara ya Afya na anayeshughulikia kufuata waliotangamana na waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.
Jumatatu, watu wanne walithibitishwa kufariki kutokana na Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Idadi hiyo imefikisha jumla ya watu 238 walioangamizwa na Covid-19 nchini, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.
Kati ya wanne hao, mwathiriwa wa umri mkubwa amekuwa na miaka 72 na ambaye Wizara ya Afya imesema aliugua maradhi ya Moyo, Kisukari na Figo. Wengine ni wenye umri wa miaka 51, 39 na 30.
Wizara ya Afya pia imethibitisha maambukizi mapya 418 kutoka kwa sampuli 2,474 zilizofanyiwa ukaguzi na vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Kufikia sasa, Kenya imefikisha jumla ya sampuli 246,361 zilizofanyiwa vipimo, na jumla ya visa 13,771 vya corona.
Kati ya maambukizi mapya ya Jumatatu, 408 ni Wakenya na 10 wakiwa raia wa kigeni, umri wa mgonjwa mdogo ukiwa mwaka mmoja na ule mkubwa miaka 86.
“Idadi ya wanaume imekuwa 263, na wanawake 155, mkondo wa wanaume kuwa waathiriwa wakuu unaendelea kushuhudiwa,” akasema Dkt Aman.
Akipigia upatu jitihada za wahudumu wa afya, Dkt Aman alisema wagonjwa 494 wamethibitishwa kupona, 465 kati yao wakiwa wanaopokea matunzo na matibabu nyumbani huku 29 kutoka vituo mbalimbali vya afya.
Takwimu hiyo inafikisha jumla ya 5,616 waliothibitishwa kupona kabisa nchini virusi vya cona.
“Ninahimiza Wakenya kwa kuwa zuio la kusafiri liliondolewa pamoja na maeneo ya kuabudu kufunguliwa, wawajibike. Huu ndio wakati wa kulinda maisha ya ndugu na dada yako, linda maisha yangu nami nilinde yako,” Waziri Aman akasisitiza, wakati akitoa takwimu hizo katika makao makuu ya idara ya afya Nairobi.