• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Mikakati iwekwe kuboresha kilimo cha pareto na kahawa, asema mbunge

Mikakati iwekwe kuboresha kilimo cha pareto na kahawa, asema mbunge

Na LAWRENCE ONGARO

WIZARA ya Kilimo inastahili kuweka sheria mpya zitakazochangia katika kufufua na kuboresha zao la pareto na kahawa.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema kwa muda mrefu wakulima wengi wa mazao hayo wamekosa kufurahia jasho lao huku wakipunjwa na mawakala.

Hata hivyo, alisema zao la pareto limekuwa halitambuliki kwa muda mrefu tangu miaka ya tisini na kwa hivyo serikali ifanye jambo kuona ya kwamba zao hilo linarudia hadhi yake ya hapo awali.

“Tayari kuna wakulima wengi ambao wangetamani kurejelea kilimo cha pareto, lakini hofu yao ni kwamba hawana soko maalum watakapouza bidhaa,” alisema Wainaina.

Alisema jukumu la kwanza liwe ni kuhimiza wakulima popote walipo waingilia upanzi wa zao hilo kwa sababu pia lina faida kubwa hapo baadaye.

Alimtaka Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya aweke mikakati na wahusika muhimu kuona ya kwamba wakulima wanapata pembejeo ili waweze kujihusisha na kilimo cha pareto.

Kuhusu kilimo cha kahawa alisema ‘dhahabu’ ya hapo awali imedorora kutokana na soko kuwa mbovu.

“Hata wakulima wa kahawa wamepoteza imani na ukuzaji wa zao hilo kwa sababu hata wakifanya bidii ya kuchuma zao hilo kutoka mashambani bado hakuna faida wanayopata,” alisema Bw Wainaina mwishoni mwa wiki mjini Thika alipokutana na wakulima kadha kutoka maeneo tofauti kutoka Kiambu.

Alipongeza juhudi zilizochukuliwa na waziri Munya kwa kuwasilisha mswada wa majanichai bungeni.

Alisema mwelekeo uliochukuliwa na waziri huyo unastahili kusukumwa pia mwingine kama huo bungeni ili kuwanufaisha wakulima wa pareto na kahawa.

“Tunajua ya kwamba nchi yetu ina wakulima wenye bidii ambao wakipewa motisha na mwelekeo ufaao bila shaka wataweza kupiga hatua kubwa kwa upande wa kilimo,” alisema mbunge huyo.

You can share this post!

Fulham wakaba Liverpool koo na kuwanyima fursa ya kutua...

Vardy na Maddison wabeba Leicester City hadi tatu-bora EPL