Miradi ya barabara hatarini Mombasa
Na WACHIRA MWANGI
HATARI inawakodolea macho raia kufuatia kuharibika kwa sehemu za miradi miwili mikubwa ya miundo msingi katika Kaunti ya Mombasa.
Kamati ya Bunge kuhusu Uchukuzi imesema maporomoko ya ardhi yamesababisha nyufa katika sehemu ya barabara ya pembeni ya Dongo Kundu na mkondo wa ndege kutua na kupaa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi (MIA).
Akiongea na wanahabari katika uwanja huo, mwenyekiti wa kamati hiyo David Pkosing alisema kuwa miradi hiyo miwili inakabiliwa na hatari ya kuharibika ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Kuna maporomoko makubwa ya ardhi ambayo yameziba kabisa sehemu moja ya barabara ya Dongo Kundu Bypass. Uwanja wa ndege pia uko hatarini kwa sababu mkondo mbadala wa kutumiwa na ndege kupaa na kutua tayari umeharibika na utahitaji kufanyiwa ukarabati.
“Baada ya miaka mingine mitano tunaweza kupoteza asilimia 25 ya mkondo huu na hautaweza kutumika tena. Hatua inapasa kuchukuliwa haraka. Njia itengenezwe ya kuruhusu maji kwenda kwenye bahari. Hii isipofanyika huenda tukapoteza uwanja huu,” akasema.
Mwenyekiti huyo alikuwa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya miundo msingi katika eneo la Pwani.
Bw Pkosing alisema sehemu za kusini na magharibi mwa uwanja wa ndege wa Moi zinakabiliwa na hatari ya kuharibika licha ya kazi nzuri ambayo inafanywa katika eneo la kaskazini mwa uwanja huo.
Barabara ya Dongo Kundu iko pembeni mwa mkondo huo wa kutua na kupaa kwa ndege na maji yote ambayo hukusanywa katika uwanja wa MIA, hupenyeza chini ya ardhi yakielekea katika Bahari ya Hindi.
Bw Pkosing alisema inaonekana kuwa mtiririko wa maji ndani ya bahari umezuiwa na akazitaka Mamlaka ya Barabara Kuu (KeNHA), Shirika la Reli Nchini na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA) kusuluhisha tatizo hilo.
“Tumetoa wito kwa asasi hizi kuandaa mkutano kujadili jinsi ya kuokoa sehemu hii muhimu wa uwanja wa ndege, barabara ya Dongo Kundu na barabara ya reli ya kisasa (SGR) ambazo zinakabiliwa na hatari ya kuangamia.
“Tumewataka wahandisi kuchunguza mfumo wa kuondoa maji kuona ikiwa mifereji inaweza kuwekwa ya kupitisha maji hadi baharini,” akasema.
Mnamo mwezi wa Julai, KeNHA ilifunga sehemu ya barabara pembeni ya Mombasa Southern bypass baada ya nyufa kuanza kuonekana katika barabara ya Miritini-Mwache-Kipevu ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kufanywa kubaini chanzo cha nyufa hizo japo mamlaka hiyo ilisema nyufa hizo zilisababishwa na masuala ya kimaumbile.
“Sehemu ya barabara hiyo inayopakana na uwanja wa MIA imechunguzwa na kubainika kuwa ina nyufa zilizotokana na mitikiso ya kijiolojia,” ikasema taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa KeNHA Peter Mundia.