Misongamano mipakani kupandisha bei ya unga
BARNABAS BII na ONYANGO K’ONYANGO
WASAGAJI mahindi nchini wamelalamikia upungufu wa mahindi kutokana na jinsi malori yalivyokwama katika maeneo ya mipaka, na kuashiria bei ya unga itapanda zaidi.
Katika juhudi za kukabiliana na janga la corona, madereva wengi wameshindwa kuvuka mipakani kwani inachukua muda mrefu kabla wapimwe na kupewa idhini ya kuingia.
Hali hii imefanya iwe vigumu kupokea mahindi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Walilalamika kuwa huenda tani kadhaa za mahindi zikaharibika katika eneo la Namanga, lililo kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania.
Tanzania imekuwa ikiwazuia madereva kutoka Kenya kuingia humo ikitilia shaka vyeti vyao kuhusu virusi, huku Kenya ikisisitiza hakuna dereva wa kutoka nje atakayeingia bila kuidhinishwa hana virusi vya corona.
Chama cha Wasagaji cha Grain Belt (GBMA), kilisema baadhi ya madereva wamekuwa wakingoja kupewa vyeti na stakabadhi muhimu za usafiri kwa karibu mwezi mmoja.
Walisema kuwa hilo pia limechangia gharama ya kusaga na kutayarisha mahindi hayo kuongezeka.
“Baadhi ya mahindi yameanza kuota kutokana na kunyeshewa na ucheleweshaji unaochangiwa na taratibu ndefu za utoaji stakabadhi katika eneo la mpakani. Hili ni jambo ambalo litawasababishia wasagaji hasara kubwa,” akasema mwenyekiti wa chama hicho, Bw Kipng’etich Mutai.
Mahindi yaliyoagizwa kutoka Tanzania yanauzwa kwa Sh2,800 kwa gunia la kilo 90 ikilinganishwa na Sh3,200 humu nchini.
“Huenda baadhi ya wasagaji wakalazimika kusimamisha shughuli zao au hata kuwafuta baadhi ya wafanyakazi wao kutokana na upungufu wa mahindi nchini,” akasema.
Pakiti ya unga ya kilo mbili inauzwa kwa Sh125 ikilinganishwa na Sh110 katika maeneo mengi katika ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa. Baadhi ya WaKenya wamelalamikia bei hiyo, wakiitaja kuwa ghali sana.
Kufikia sasa, wasagaji wameagiza tani 60,000 za mahindi ambazo bado hazijaanza kuuzwa kutokana na kesi iliyowasilishwa mahakamani na mwanaharakati Okiya Omtatah.
Kwenye kesi hiyo, mwanaharakati huyo anataka wasagaji kuzuiwa kuagiza mahindi, akilalamikia ubora wake.
Kando na wasagaji, amezishtaki wizara za Kilimo na Fedha.
Kesi pia inamaanisha kuwa mahindi yaliyoagizwa kutoka Mexico yatakaa sana yatakapowasili katika Bandari ya Mombasa kabla ya kuingizwa nchini.