• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Mitumba yarejea sokoni Thika kwa kishindo

Mitumba yarejea sokoni Thika kwa kishindo

Na LAWRENCE ONGARO

WAUZAJI wa nguo za mitumba mjini Thika, Kaunti ya Kiambu, walipata afueni baada ya serikali kuwapa ruhusa ya kuendelea na biashara hiyo.

Biashara ya nguo za mitumba ilisitishwa na kwa kiasi fulani kuyumba kuanzia mwezi Aprili 2020, kufuatia mlipuko wa homa ya Covid-19.

Baada ya waandishi wa habari kuzuru vituo kadha vya kuuzia bidhaa hiyo, ilibainika ya kwamba wakazi wa Thika walifurika maeneo hayo ili kujichagulia nguo hizo.

Muuzaji wa nguo za mitumba Bi Jane Kabaria aliishukuru serikali kwa kuwaruhusu kuendelea na biashara hiyo baada ya kukosa kazi kwa kipindi cha miezi minne hivi.

“Wengi wetu tulikuwa katika hali ngumu kimaisha kwa sababu hadi sasa hatujalipa kodi za nyumba. Wengine pia walikosa chakula cha kila siku,” alisema Bi Kabaria.

Kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake alisema wanafuata maagizo ya Wizara ya Afya kwa kunawa mikono, kuvalia barakoa na cha muhimu kabisa kuweka nafasi ya umbali wa mita chache kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwenzake.

Hata hivyo, wafanyabiashara wanaouza nguo mpya za dukani watapata pigo kwa sababu watu wengi wamerejea kununua nguo za mitumba.

Mikopo nafuu

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alisema wengi wamepata hasara kubwa ambapo serikali inastahili kuwajali kwa kuwapa mikopo ya kujikwamua kifedha.

Mkazi wa Thika John Kamau alisema hakuweza kununua nguo mpya za kutoka dukani, lakini baada ya serikali kuruhusu nguo za mitumba kuendelea kuuzwa, “sasa nitaweza kupata nguo ya bei nafuu.”

Baada ya serikali kukubalia nguo za mitumba kuuzwa sokoni, wafanyabiashara wengi wanaouza nguo za dukani watapata pigo kwa sababu watu wengi sasa wamerudia nguo za mitumba ambazo walizoea kuvalia hapo awali.

Mkazi wa Juja Bw Peter Karanja anasema tangu kufungwa kwa biashara ya  mitumba miezi minne iliyopita, hajawahi kununua nguo yoyote kwani hangeweza kugharimia nguo mpya ya dukani.

“Sasa wananchi wa kawaida wataweza kupata nguo za bei nafuu za mitumba; na kwa hivyo tunapongeza serikali kwa kazi njema waliyofanya ya kufungulia biashara hiyo kote nchini,” alisema Bw Karanja.

You can share this post!

Akana kuiba kuku 152

Ashtakiwa kuiba mafuta ya injini