Habari Mseto

Mjane akana kuiba Sh150m

August 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MJANE alishtakiwa Jumanne kwa kughushi saini ya nyanya wa miaka 70 na kupokea mkopo wa Sh150 milioni kutoka kwa benki ya Faulu.

Bi Esther Muthoni Njoroge alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani kwa kughushi saini ya Bi Alice Wanjiru Wamwea na kutia saini Fomu za kupokea mkopo.

Bw Andayi alielezwa na kiongozi wa mashtaka kwamba kesui hiyo dhidi ya Muthoni itaunganishwa na nyingine ambapo washukiwa wengine watano wameshtakiwa wakiwamo wafanyakazi watatu wa Benki ya Faulu.

“Kesi hii itaunganishwa na nyingine dhidi ya maafisa watatu wa benki ya Faulu walioshtakiwa wiki iliyopita,” alisema kiongozi wa mashtaka.

Hakimu alielezwa kuwa mshtakiwa alikuwa mgonjwa na angelifika mahakamani wiki iliyopita.

“Muthoni na mshukiwa mwingine Tom Jaseme walikuwa wameagizwa wajisalamishe katika afisi ya uchunguzi wa jinai (DCI) katika kituo cha polisi cha Muthaiga Alhamisi wiki iliyopita,” hakimu alifahamishwa.

Mahakama ilijulishwa mshtakiwa alijisalamisha kwa afisi hiyo ya DCI katika kituo cha Polisi cha Muthaiga Jumatatu alipopata nafuu.

“Mshtakiwa yuko na mtoto mdogo wa miaka sita na ndiye anayewatunza wazazi wake wazee. Hawezi kutoroka. Alijisalamisha kwa polisi kwa hiari na akaandika taarifa,” wakili aliyemkwakilisha Muthoni alimweleza hakimu.

Mahakama iliombwa imwachilie kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu kama washukiwa walioshtakiwa wiki jana.

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu na kuamuru kesi hiyo iunganishwe na hiyo inayowakabili washtakiwa wengine.

Walioshtakiwa wiki iliyopita mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kenndy Cheruiyot ni Amos Muigweru Mwangi, Peter Kefa Onsongo na Tom Jasema.

Amos Muigweru Mwangi, Peter Kefa Onsongo, Paul Njuki na Tom Jasema. Picha/ Richard Munguti

Walikanusha shtaka la kufanya njama za kumlaghai Bi Wamwea jumba lake la kibiashara kinyume cha sheria lililo na thamani ya Sh150milioni.

Jumba hilo liko katika mtaa wa Huruma Nairobi. Watatu hao walishtakiwa pamoja na dalali Robert Waweru Maina na Bi Esther Muthoni Njoroge.

Sita hao walishtakiwa pamoja na kampuni ya Hosana Investments Limited na Antique Auctions Agencies.

Shtaka la kwanza likuwa dhidi ya wanabenki hao watatu,dalali na Bi Njoroge.

Walidaiwa kati ya Mei 30 2015 na March 28 2018 walifanya njama za kuuza jumba la Ni Wamwea lenye thamani ya Sh150,000,000.

Shtaka la pili lilikuwa dhidi ya Amos Mwangi. Alidaiwa kati ya Agosti 8 2014 na Aprili 11 2015 katika makao makuu ya benki ya Faulu jijini Nairobi akishirikiana na wengine ambao hawajashtakiwa aliiba Sh22milioni.

Shtaka la tatu lilikuwa dhidi ya Esther Muthoni na lilisema kuwa mnamo Mei 23 2015 alighushi saini ya Bi Wamwea na kuomba mkopo kutoka kwa benki ya Faulu.

Kesi imeorodheshwa kusikizwa Septemba 18, 2019.