Habari Mseto

Mkaguzi bandia wa mita za Kenya Power anaswa

August 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) jijini Nairobi wamemkamata mwanamume mmoja ambaye alikuwa akipanga kumlaghai mteja mmoja pesa akijifanya kuwa afisa wa kukagua mita za kampuni ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power.

Kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa twitter tume hiyo Jumanne ilisema kuwa: “mwanamume huyo kwa jina Michael Njogu Mburu aliitisha hongo ya Sh200,000 ili aziue hatua za kinidhamu dhidi ya malalamishi ambaye alimpata na hatua ya kuvuruga mita ya stima.”

EACC ilisema mshukiwa huyo atafikishwa katika mahakama ya milimani Jumatano.

Haya yanajiri baada ya mwanamume mwingine kukamatwa jana asubuhi akiwa na mali ya Kenya Power, ikiwemo nyaya za stima, kwenye operesheni iliyoendeshwa katika mtaaa wa Membley, Ruiru, kaunti ya Kiambu.

Polisi walisema mali hiyo, ya thamani ya mamilioni ya fedha, ilipatikana ikiwa imehifadhiwa katika nyumba moja mtaani humo.

Maafisa hao walisema mshukiwa alikamatwa baada ya kupatikana akisafirisha baadhi ya nyaya hizo, zinazoaminika kuwa mali ya Kenya Power.

Uchunguzi unaendelea kubaini jinsi mali hiyo ilitolewa kutoka kwa hifadhi ya kampuni hiyo kwa lengo la kuwanasa wahusika wote katika wizi huo.