• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Mkate wasababisha msongamano kivukoni Likoni

Mkate wasababisha msongamano kivukoni Likoni

Na MISHI GONGO

MKURUGENZI mkuu katika shirika la huduma za feri nchini Bw Bakari Gowa amesema kuwa idadi ya wa wanaotumia kivuko cha Likoni imepungua maradufu tangu kuzuka kwa janga la corona huku akibainisha msongamano unaoshuhudiwa kwa sasa ni wa wale wanaotafuta chakula.

Akiongea katika mahojiano na kamati ya seneti kuhusu janga la corona inayoendeleza ziara yake Pwani, alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya watu kupoteza ajira katika viwanda mbalimbali vilivyoko Mombasa Kisiwani.

Ziara hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Bi Sylvia Kasanga ambaye aliandamana na Seneta wa Kaunti ya Kwale Issah Boy, Mohammed Faki (Mombasa), Mithika Linturi (Meru) na Abshiro Halake (Isiolo) ni ya kuangalia jinsi kaunti zinavyoendeleza vita dhidi ya virusi hivyo hatari.

Kulingana na Bw Gowa, msongamano ulitokana na wenyeji wanaoenda katika shughuli kadhaa hasa vibarua kila siku lakini tangu kuzuka kwa janga la corona, watu wengi walipoteza ajira kufuatia baadhi ya viwanda kufungwa.

“Tangu kuzuka kwa janga la corona idadi ya watu wanaotumia kivuko hiki imepungua. Wengine walikuwa wanavuka kwenda kufanya gange katika viwanda mbalimbali,” akasema.

Alisema msongamano unaoshuhudiwa kwa sasa ni ule wa watu wanaovuka kutoka upande wa nchi kavu kusaka mlo.

Kutoka kushoto ni Seneta wa Kaunti ya Mombasa Mohammed Faki, naibu mwenyekiti wa kamati ya seneti kuhusu Covid-19 Bw Mithika Linturi, mwenyekiti wa kamati ya seneti ya Covid-19 Bi Sylvia Kasanga halafu mwisho ni Mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Bw Mahmoud Noor. Picha/ Mishi Gongo

Alisema msongamano huo huwa wanapambana nao siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.

“Wanawake na watoto mnaowaona wakivuka wanaenda kupokea chakula kinachotolewa na usimamizi wa kampuni ya kutengeneza simiti ya Bamburi,” akasema.

Alisema hali ngumu ya maisha imesababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaoenda kupokea chakula hicho.

Bw Gowa alisema kwa sasa wanaendeleza majadiliano na kampuni hiyo kuona kuwa ufadhili huo unapelekwa upande wa nchi kavu kupunguza msongamano huo.

Hata hivyo, alisema kampuni ya Bamburi ilisema mwanzo inapanga kuimarisha usalama wa wafanyakazi wao kabla ya kuweka kambi upande huo.

“Wanapopeana mikate hutokea mvurugano na hata kuna wakati mfanyakazi wao mmoja aliumizwa alipokuwa anagawa chakula,” akasema Bw Gowa.

Seneta wa Isiolo Bi Abshiro Halake alieleza kusikitishwa na hali ya wanawake kutembea mwendo mrefu kufuata mikate.

You can share this post!

Bima ya afya bado ghali kwa Wakenya, lakini suluhu zipo

Mwili wa mwanamke aliyekufa maji waendelea kusakwa