Mke alimsukuma mwanangu baharini, mama sasa alia
NA KITAVI MUTUA
FAMILIA ya mwanamme aliyefariki baada ya kujitosa katika Bahari Hindi akiwa ndani ya gari lake wikendi iliyopita ilisimulia jinsi alivyokuwa amevumilia miaka mingi ya dhuluma katika ndoa kutoka kwa mkewe.
Huku wakijiandaa kumzika, mamake John Mutinda, Bi Musangi Mutinda alijitokeza kumshutumu mkaza mwanawe dhidi ya kubuni uongo na ufafanuzi usio wa kweli ili kuficha dhuluma alizokuwa amemtendewa mumewe kisiri.
Katika mahojiano na Taifa Leo nyumbani mwake katika kijiji cha Kyanika, Kaunti ya Kitui, mama huyo aliyejawa na simanzi alifichua kuwa mwanawe alikuwa akipokea nafuu kutokana na majeraha mabaya aliyosababishiwa na mkewe aliyemchoma kwa maji moto mwezi uliopita.
“Mwanangu alifariki kutokana na msongo wa mawazo na kukata tamaa hali iliyotokana na dhuluma za kinyumbani na masaibu ya ndoa aliyovumilia nyumbani. Kwa hivyo ni vibaya kwa mkewe kunuiza kwamba alikuwa ameingiwa na kichaa,” alisema Bi Mutinda.
Huku akishika picha za mwanawe aliyejawa vidonda kote kifuani mwake, Bi Mutinda alisema uongo wa mkaza mwanawe ulikuwa umeongeza uchungu kuhusu kifo cha baba huyo wa watoto watatu.
Mhasiriwa alifululiza kutoka nyumbani kwake Eneo la Vanga, Likoni, Kaunti ya Mombasa mwendo wa saa kumi alfajiri, akaabiri gari lake na kuelekea kwa kasi katika kivukio cha Likoni kabla ya kujitumbukiza baharini.
Mkewe, Bi Ruth Mueni baadaye alidai kuwa mumewe, aliyekuwa ajenti wa kupakia na kupakua alianza kuwa na tabia zisizo za kawaida usiku huo baada ya kupokea simu isiyo ya kawaida kutoka kwa marehemu babake aliyefariki miaka mingi iliyopita.
Jana, Bi Mueni alikiri walikuwa na matatizo ya ndoa lakini akasisitiza vyombo vya habari vinapaswa kumruhusu amwomboleze marehemu mumewe kwa amani.
Alikataa kujadili ni kwa nini alimchoma mumewe kwa maji moto akisema tu alihitaji muda kufafanua hali kwa mama mkwe wake na jamaa wengine wa familia waliokuwa wakilalamika kumhusu.
“Nani amekupa picha hizo? Hili ni suala la kibinafsi la kifamilia na siwezi kuzungumza kwa sasa maadamu niko katika kituo cha polisi nikiandaa shughuli ya upasuaji,” alisema.
Madai ya mamake marehemu yalithibitishwa na ndugu zake marehemu waliojutia kutoingilia kati mapema ili kumnusuru dhidi ya kukata tamaa maishani.