• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 1:16 PM
Mke na mume washtakiwa kwa ulaghai unaohusu biashara ya parachichi

Mke na mume washtakiwa kwa ulaghai unaohusu biashara ya parachichi

Na RICHARD MUNGUTI

DADAYE mwanasiasa Steve Mbogo, Bi Jennifer Mukonyo Mbogo alishtakiwa Ijumaa pamoja na mumewe kwa ulaghai wa Sh18.5 milioni katika biashara ya kuuza parachichi ng’ambo.

Jennifer pamoja na mumewe Nathan Loyd Ndung’u walikabiliwa na mashtaka 13 ya kula njama za kulaghai na kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu kati ya Machi 1 na Aprili 1, 2020.

Wawili hawa, inadaiwa walikula njama kuilaghai kampuni ya Ezetel Kenya Limited mamilioni ya pesa wakidai walikuwa na uwezo wa kushirikiana nayo kufadhili na kufanikisha uuzaji wa matunda hayo ng’ambo.

Jennifer na Nathan ni wakurugenzi wa kampuni ijulikanayo kwa jina Avo-veg Health Kenya Limited.

Wawili hawa inadaiwa waliieleza kampuni ya Ezetel kwamba wao kama wakurugenzi wa Avo-veg Health Kenya Limited walikuwa na uwezo kushirikiana nayo katika mauzo ya parachichi kutoka humu nchini hadi nchi za kigeni.

Pia wawili hao wanakabiliwa na shtaka la kutoa hundi 13 ambazo zilikataliwa na benki.

Hundi hizo wanazoshtakiwa kutumia kuilipa Ezetel zilikuwa za Sh990,000 mnamo Machi 28 2020.

Mahakama ilielezwa na kiongozi wa mashtaka kuwa hundi hizo zilikuwa zilipwe Ezetel na Benki ya SBM lakini washtakiwa walikuwa wameiagiza benki hiyo isithubutu kulipa.

Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi alielezwa lengo la wawili hao ilikuwa kuilaghai kampuni hiyo pesa.

Washtakiwa hao waliokanusha shtaka walimweleza hakimu kupitia wakili wao Bi Mercy Kinyua kwamba kesi hiyo inatokana na mzozo wa kibiashara na unaweza ukaamuliwa na Mahakama Kuu inayoshughulikia kesi za kibiashara.

“Kesi hii haifai kuwa ya uhalifu kwa vile inatokana na muwafaka wa kibiashara,” Bi Kinyua alifichua mbele ya hakimu.

Wakili huyo alieleza mahakama kwamba kufikia sasa washtakiwa hao wamelipa Ezetel na tayari kuna hundi ya Sh5 milioni iliyotolewa kwa kampuni hiyo.

Mahakama iliombwa iwaachilie wawili hao kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu huku hakimu akifahamishwa washtakiwa wameacha watoto wadogo nyumbani.

Wawili hao walimweleza Bw Ochoi kwamba hawakuila njama za kuifuja Ezetel.

Walisema wako na makazi jijini Nairobi na wako na biashara wanazofanya na kwamba wao hawatachana mbuga wakiachiliwa kwa dhamana.

Lakini wakili wa kampuni hiyo ya Ezetel alikana wawili hao waliilipa pesa hizo wanazodai.

Ezetel ilieleza korti kuwa wawili hao ni wajanja kwa vile ilichukua muda mrefu kwa maafisa wa usalama kuwatia kuwafikia washukiwa kuwahoji na hatimaye kuwafikisha mahakamani.

Bw Ochoi aliamuru washtakiwa hao wazuiliwe rumande hadi Jumatatu, Julai 20, 2020, atakapoamua iwapo atawaachilia kwa dhamana au la.

Bw Ochoi aliamuru idara ya urekebishaji tabia iwahoji wawili hao na kuwasilisha ripoti mahakamani kabla ya uamuzi wa iwapo wataachiliwa kwa dhamana au la.

You can share this post!

RIZIKI: Jinsi unavyoweza kujiimarisha kimapato kupitia...

Aliyejifanya polisi atiwa nguvuni

adminleo